Serikali yajipanga kufikisha Nishati safi ya kupikia kila Kaya Nchini



Na Mwandishi wetu, Geita

Wizara ya Nishati kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imejipanga kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia yanafikia kila kaya nchini ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kulinda afya za wananchi na kuhifadhi mazingira.

Akizungumza katika mahojiano maalum wakati wa Maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, Mhandisi Evance Kabingo alisema Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha wananchi wanatumia nishati salama, isiyo na madhara kwa afya wala mazingira.

“Serikali imepanga kufanikisha matumizi ya nishati safi kwa angalau asilimia 80 ya wananchi ifikapo mwaka 2030. Hii ni pamoja na gesi asilia (LPG), umeme, na majiko ya kisasa yenye teknolojia rafiki kwa mazingira,” alisema Mhandisi Kabingo.

Aliongeza kuwa matumizi ya nishati chafu kama kuni na mkaa yamekuwa chanzo kikuu cha matatizo ya kiafya kwa akina mama na watoto pamoja na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti hovyo.

Mhandisi Kabingo alisema Serikali kwa kushirikiana na mamlaka za Serikali za mitaa, sekta binafsi na wadau wa maendeleo, inaendesha kampeni za uhamasishaji kuhusu faida za kutumia nishati safi pamoja na kusambaza vifaa vya kupikia kwa gharama nafuu.

Aidha, REA imeanzisha mpango wa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya gesi na majiko banifu ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.

“Tunatumia fursa ya maonyesho haya kuwaelimisha wananchi na wafanyakazi wa migodi kuhusu matumizi ya nishati safi. Lengo letu ni kulinda mazingira na afya za wananchi,” alisema.


Katika maonyesho hayo, REA imetoa majiko banifu na mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku. Takribani wananchi 1,500 wanatarajiwa kufikiwa ifikapo mwisho wa maonyesho hayo.

Kwa mujibu wa utaratibu huo, mwananchi huchangia asilimia 35 ya gharama ya jiko la gesi, huku Serikali ikigharamia asilimia 65. Kwa majiko banifu, wananchi hulipia shilingi 6,200 pekee kati ya bei halisi ya shilingi 41,300, Serikali ikigharamia asilimia 85 ya gharama.

Wananchi waliotembelea banda la REA wameipongeza Serikali kwa mpango huo wa ruzuku.

Nasra Makungu, mkazi wa Ujamaa, Geita alisema:
“Kabla ya mpango huu, wengi hatukuwa na uwezo wa kununua majiko ya gesi. Lakini sasa, kwa shilingi 6,200 unaweza kupata jiko la kisasa. Ni msaada mkubwa sana.”



Naye Pelagia Paschal wa Nyaukumbu alisema:
“Bei ya kawaida ya majiko ilikuwa kikwazo kwa wananchi wa kipato cha chini. Kwa shilingi 6,200 kwa jiko banifu na shilingi 17,500 kwa mtungi mdogo, sasa tumewezeshwa. Tunaishukuru Serikali.”


Mhandisi Kabingo amewahimiza wananchi kuendelea kujitokeza kupata elimu na vifaa hivyo, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha matumizi ya nishati safi kwa maendeleo endelevu ya jamii.

Previous Post Next Post