DC KINGALAME AIPONGEZA TBA KWA MRADI WA MAKAZI YA BIASHARA GEITA




Na Mwandishi Wetu, Geita

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame, ameipongeza Taasisi ya Nyumba Tanzania (TBA) kwa kuja na wazo la kuanzisha mradi mkubwa wa Makazi ya Biashara mkoani Geita, akisema mradi huo ni kielelezo cha tafsiri ya maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora.

Akizungumza Septemba 24, 2025, alipotembelea maonyesho ya nane ya Teknolojia ya Madini katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili mkoani Geita, Kingalame alisema uamuzi huo wa TBA ni hatua muhimu ya kuimarisha ustawi wa wananchi kupitia miradi ya kimkakati ya makazi.

“Nimekuja kushuhudia wazo hili la kuanzisha mradi mkubwa wa Makazi ya Biashara mkoani Geita. Hii ni tafsiri ya maono ya Rais Dkt. Samia, anatamani watu wake wakae kwenye maeneo mazuri na yenye hadhi,” alisema Kingalame.


Aidha, alitoa pongezi kwa TBA kwa uamuzi wa kukaribisha sekta binafsi kushirikiana nao, akisema ushirikiano huo utasaidia kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyohitajika.

“Naomba sekta binafsi ichangamke kushirikiana na TBA ili makazi haya yakamilike kwa muda muafaka. Hii italeta raha kwa sababu watumishi na wananchi kwa ujumla watapata makazi bora ya kuishi,” alisisitiza.

Mradi huo wa Makazi ya Biashara mkoani Geita unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, huku ukitarajiwa kuongeza thamani ya mji wa Geita na kutoa suluhisho la changamoto za makazi kwa wananchi na watumishi wa umma.
Previous Post Next Post