GCAP YAIOMBA SERIKALI KUWEKA MISINGI WA MAENDELEO JUMUISHI NA HAKI ZA BINADAMU





Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Serikali ya Tanzania imetakiwa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) unaleta manufaa kwa wananchi wote, hasa makundi yaliyo pembezoni, huku haki za binadamu zikipewa kipaumbele.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Rosemary Mwaipopo kutoka shirika la Dayspring Foundation, ambaye pia ni mjumbe wa mtandao wa GCAP (Global Call to Action Against Poverty), wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya wanaharakati, wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na jamii za vijijini.

Mwaipopo alisema kuwa miaka 10 ya utekelezaji wa SDGs imeleta mafanikio fulani, lakini bado changamoto nyingi zinahitaji kushughulikiwa kwa dharura na kwa pamoja na wadau wote wa maendeleo.




“Ni wakati wa hatua thabiti na jumuishi. Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia, mashirika ya kimataifa na wananchi wote kwa ujumla, tunapaswa kushirikiana kwa vitendo kuhakikisha maendeleo yanamfikia kila Mtanzania, bila kumwacha yeyote nyuma,” 

Miongoni mwa maeneo yaliyosisitizwa ni pamoja na kulindwa kwa haki za raia, kuimarishwa kwa misingi ya utawala bora, pamoja na kuongeza uwekezaji katika sekta za huduma za jamii kama afya, elimu, maji safi na nishati mbadala.

Mwaipopo alitaka sera na bajeti za taifa zijikite zaidi kwenye uchumi jumuishi unaowezesha upatikanaji wa ajira zenye staha kwa vijana na wanawake, sambamba na kuweka mifumo ya hifadhi ya jamii inayowafikia wananchi walio katika mazingira magumu.



Katika mkutano huo, asasi za kiraia (AZAKI) zilitakiwa kuendelea kuwa sauti ya wananchi kwa kufuatilia utekelezaji wa SDGs na kushirikiana kwa mshikamano katika kudai uwajibikaji na usawa wa kijamii.

Umoja wa Mataifa na taasisi za kikanda ziliombwa kuongeza msaada wa kiufundi, kifedha na rasilimali kwa Tanzania ili kuchochea utekelezaji wa malengo ya maendeleo. Pia, nchi tajiri zimetakiwa kutimiza ahadi zao za ufadhili wa maendeleo na fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Sekta binafsi nayo ilihimizwa kuwekeza katika biashara jumuishi, kutoa mafunzo ya ajira kwa vijana na kuhakikisha uwekezaji unazingatia usawa wa kijinsia na hifadhi ya 

Aidha, wananchi waliombwa kushiriki kikamilifu katika mijadala ya maendeleo, kuwawajibisha viongozi, na kuwa mstari wa mbele katika kulinda mazingira pamoja na kudai haki za kijamii na kiuchumi.

> “Maendeleo ya kweli yanahitaji ushirikishwaji wa kila mmoja wetu. Tusibaki kuwa watazamaji, bali tuwe sehemu ya suluhisho,” aliongeza Mwaipopo.






Kwa upande wake, Martina M. Kabisama, mwakilishi wa GCAP Tanzania Coalition, alisema licha ya hatua kadhaa za maendeleo kufikiwa katika sekta kama elimu, afya na miundombinu, changamoto za umasikini, ukosefu wa ajira rasmi, na usawa wa kijamii bado ni kubwa.

Alieleza kuwa Tanzania imezindua Dira ya Maendeleo 2050 ambayo inalenga kujenga uchumi shindani na jumuishi, kuongeza umri wa kuishi hadi miaka 75 na kuhakikisha zaidi ya asilimia 90 ya kaya zinapata huduma za nishati. Hata hivyo, alionya kuwa mafanikio haya hayawezi kufikiwa iwapo usawa na haki havitawekwa mbele.

Ripoti ya GCAP inaonyesha kuwa ingawa umasikini umepungua kutoka asilimia 34.4 mwaka 2007 hadi asilimia 26.4 mwaka 2017/18, zaidi ya asilimia 14 ya Watanzania bado wanaishi kwenye umasikini uliokithiri. Zaidi ya vijana 800,000 wanaoingia sokoni kila mwaka, asilimia 80 huishia kwenye sekta isiyo rasmi isiyokuwa na ulinzi wa kijamii.

Mabadiliko ya Tabianchi na Ukosefu wa Uwajibikaji Vyaathiri Maendeleo

Miongoni mwa changamoto nyingine zilizotajwa ni athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kilimo, ukosefu wa ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi ya maendeleo, pamoja na ukosefu wa uwazi katika usimamizi wa rasilimali.

 “Ukuaji wa uchumi wa asilimia 5 haujaweza kuwafikia wananchi wote kwa usawa. Pengo kati ya matajiri na maskini linaendelea kupanuka,” aliongeza Kabisama.



Aidha, huduma za hifadhi ya jamii bado ni finyu, ambapo ni chini ya asilimia 12 ya Watanzania wanaofikiwa na huduma hizo. Mpango mkubwa wa TASAF umeweza kufikia kaya milioni 1.5 pekee—idadi isiyokidhi uhitaji uliopo.



Kwa pamoja, GCAP na wadau wake wanasisitiza kuwa suluhisho la changamoto hizi ni kuwepo kwa mwelekeo mpya wa maendeleo unaojikita katika usawa, haki, na uwajibikaji. Wanatoa wito wa kushirikiana katika kujenga mfumo wa maendeleo unaoweka wananchi mbele na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha mafanikio ya kweli.

Previous Post Next Post