Na mwandishi wetu...
Waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam wamepata mafunzo ya muhimu kuhusu namna ya kuripoti Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kwa kuzingatia usalama wao, usawa wa kijinsia, na sheria mpya za uchaguzi zilizopitishwa mwaka 2024. Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Kampuni ya Media Brains, kwa udhamini wa Shirika la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) kutoka Ujerumani, yalilenga kuwapa wanahabari mbinu bora za kutekeleza majukumu yao bila kuvunja sheria na kuepuka upendeleo wa kijinsia.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Media Brains, Jesse Kwayu, alisema kuwa tafiti zinaonyesha kwamba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, wagombea wanawake walipata nafasi ndogo kwenye vyombo vya habari ikilinganishwa na wagombea wa kiume. Hii ni changamoto inayohitaji kushughulikiwa kwa nguvu kubwa katika Uchaguzi Mkuu ujao.
“Tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Vyombo vya habari vinapaswa kutoa nafasi sawa kwa wagombea wote, bila kuonesha upendeleo wa kijinsia,” alisema Kwayu, akisisitiza umuhimu wa usawa katika kuripoti habari za uchaguzi.
Mkurugenzi Mwenza wa Media Brains na mwandishi mkongwe, Absalom Kibanda, aliweka wazi umuhimu wa wanahabari kusoma kwa makini Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, pamoja na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
“Sheria hizi zimeanza kutumika katika mchakato wa awali wa uchaguzi. Ni muhimu wanahabari kuzifahamu ili kujilinda kisheria na kutekeleza majukumu yao kwa weledi,” alisema Kibanda.
Aidha, Mkurugenzi wa Media Brains, Neville Meena, alieleza kwamba uelewa wa sheria hizi utasaidia wanahabari kuepuka makosa, hasa wanapokuwa wanahoji wagombea na wadau mbalimbali wa uchaguzi. Uwazi na uadilifu katika kuripoti habari utaleta amani na ustawi wa demokrasia nchini.
Mafunzo hayo pia yalijikita katika umuhimu wa uhakiki wa habari kabla ya kuchapishwa, ili kuepuka kueneza taharuki na kuchochea chuki miongoni mwa jamii. Wanahabari walihimizwa kuhakikisha kwamba habari wanazozitangaza zinakuwa za kweli, sahihi na za kuzingatia maslahi ya umma.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yalijikita katika kuandaa wanahabari kukabiliana na changamoto za uchaguzi, ili kuhakikisha kwamba wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kwa usawa, na kwa usalama wao binafsi. Hii ni hatua muhimu katika kuimarisha mchakato wa uchaguzi na kulinda haki za kisiasa za wananchi wote.