NIT YAPATA ITHIBATI KUTOKA WAKALA WA USALAMA WA ANGA ULAYA




Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema kuwa Serikali kupitia Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT kwa kushirikiana na Athens Aviation Training Organization ya Ugiriki imepata ithibati kutoka Wakala wa Usalama wa Anga wa Ulaya (European Aviation Safety Agency - EASA) ya kuwa Kituo cha Mitihani ya Leseni za Kimataifa kwa Wahandisi Matengenezo ya Ndege ( EASA part – 66 Aircaft Maintenance License Training).

Akizungumza leo Alhamisi, Mei 15, 2025, bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/26, Profesa Mbarawa amesema kuwa Chuo cha NIT kitakuwa vile vile Kituo cha Mafunzo ya Uhandisi Matengenezo ya Ndege (EASA Part -147 Maintenance Training Organization).

“Mafanikio haya ni ya kipekee na ya aina yake kwa nchi yetu na yatawezesha wataalam wetu kuwa na ubora na vigezo stahiki vya ushindani wa soko la ajira kikanda na kimataifa,” amesema Waziri Mbarawa.

Ameongezea, “Serikali kupitia Chuo cha NIT imepata ithibati ya kuanza mafunzo ya Urubani kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA). Mafunzo haya yanatarajia kuanza rasmi mwezi Juni 2025.”

Ametabanaisha kuwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kimeendelea kutoa Mafunzo ya kozi ndefu 48 za kimkakati ili kuzalisha wataalam mahiri wa kuendeleza miradi mikubwa ya kitaifa inayotekelezwa naSerikali.

“Chuo kina wanafunziwakozindefu 17,701 ikilinganishwanawanafunzi 16,131 kwamwaka 2023/24, ikiwanisawanaongezeko la asilimia 9.7,” alisema Bungeni hii leo.

Alisisitiza kuwa Serikali kupitia Chuo cha NIT imeendelea kutekeleza mradi wa kuboresha miundombinu na vifaa vya kufundishia ikiwemo uundwaji wa ndege moja (1) yenye injini mbili (2) kwa ajili ya kufundishia marubani unaendelea kiwandani nchini Marekani na unatarajiwa kukamilika na ndege kuwasili Chuoni mwezi Oktoba 2025.

“Serikali kupitia Chuo cha NIT imeendelea na utekelezaji wa mradi wa uanzishwaji wa Kampasi ya NIT Lindi kwa ajili ya kuzalisha Nguvukazi Mahiri na kujenga uwezo wa kiteknolojia katika sekta ya usafiri majini, mafuta na gesi,” alisema.

Aliendelea kusema kuwa Chuo cha NIT kinaendelea na utekelezaji wa shughuli za uanzishwaji wa Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji kitakachoanzishwa chini ya Mradi wa East Africa Skills for Transformation and Regional Intergration Project (EASTRIP) ambapo kimeshatekeleza kazi mbali mbali.

“Chuo kimeshatekeleza ujenzi wa majengo matano (5) yanayojengwa katika Kampasi ya Mabibo – Dar es Salaam ambapo Mabweni mawili (2) yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,504 umekamilika na ujenzi wa majengo matatu (3) yenye madarasa 10, maabara 15, karakana tano (5) na ofisi za watumishi 25 umefikia asilimia 96,” alisema.

Mambo mengine yaliyotekelezwa kwa mujibu wa Waziri Chuoni hapo ni pamoja na ujenzi wa jengo la Karakana ya Matengenezo ya Ndege (Aviation Hangar) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) itakayotumika kuhifadhia ndege za mafunzo ya urubani na matengenezo ya ndege hizo pamoja na mafunzo ya uhandisi wa matengenezo ya ndege upo kwenye hatua ya kumpata Mkandarasi.

“Wameshafanya ununuzi wa vifaa vya mafunzo ya urubani na uhandisi wa matengenezo ya ndege ikiwemo Flight Simulators mbili (2) na programu za Kompyuta (softwares) kwa ajili ya maabara, madarasa na ofisi katika Kampasi ya NIT Mabibo – Dar es Salaam na KIA umefikia asilimia 70,” alimalizia Waziri Profesa Mbarawa.

Mwisho
Previous Post Next Post