THE RUNNERS TANZANIA YAZINDUA ABSA DAR CITY MARATHON 2025







Na Mwandishi wetu....

The Runners Tanzania wamezindua rasmi Absa Dar City Marathon 2025, ikiwa ni msimu wa tano wa mbio hizo, zitakazofanyika Mei 4, 2025, katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam. Lengo kuu la mbio hizi ni kusaidia mahitaji ya Hospitali ya Mnazi Mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Godfrey Mwangungulu, Makamu Mwenyekiti wa Runners Club, amesema wanatarajia washiriki wasiopungua 3,000 msimu huu na amewasihi watu kuendelea kujisajili kwa ada ya shilingi 40,000.

“Tunakwenda kufanya msimu wa tano wa Dar City Marathon, mbio ambazo zimekuwa zikifanyika kwa mafanikio na kuendelea kukua mwaka hadi mwaka. Mwaka huu tunatarajia washiriki zaidi ya 3,000,” alisema Mwangungulu.

Aliendelea kusisitiza kuwa mbio hizi si za mashindano tu, bali pia ni fursa ya kujenga mshikamano na kusherehekea pamoja.

Kwa upande wake, Aron Luhanga, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Absa Bank, amesema benki hiyo kama mdhamini mkuu imejipanga vyema kuunga mkono mbio hizo.




“Kaulimbiu yetu ni ‘Tunathamini Story Yako,’ na tunaamini hakuna mtu anayeweza kuandika hadithi nzuri bila kuwa na afya njema. Afya bora ndiyo msingi wa mafanikio,” alisema Luhanga.

Naye Juma Patrice, Mkuu wa Kitengo cha Bima kupitia Taasisi za Fedha, Alliance Life Assurance Limited, amesema wamekuwa wadau wa mbio hizi tangu zilipoanzishwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo hushiriki kila mwaka. Amewahimiza wakazi wa Dar es Salaam kujisajili na kushiriki mbio hizo kwa manufaa ya afya na jamii.

“Mbio hizi si tu za kusaidia Hospitali ya Mnazi Mmoja, bali pia zinahamasisha watu kufanya mazoezi, kujenga afya bora, na hata kuutambua mji wetu wa Dar es Salaam kwa mtazamo wa utalii wa ndani,” alisema Patrice.

Felix Donald, Kiongozi wa Kamati Tendaji wa Shirikisho la Urais Tanzania, amepongeza The Runners kwa kushirikiana na Absa Bank kuandaa mbio hizi kwa mara ya tano.

“Mbio hizi zinachangia maendeleo ya afya, utalii, na kusaidia jamii. Ni muhimu kuendelea kuziboresha kila mwaka,” alisema Donald.

Naye Epson Elias kutoka Kilimanjaro Fresh ameushukuru uongozi wa Dar City Marathon kwa kuwawezesha kuwa sehemu ya mbio hizo na kuwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki, kama njia ya kurudisha shukrani kwa jamii.





Previous Post Next Post