Na Mwandishi wetu....
.
Wasanii wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima afya zao wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo itakayofanyika hivi karibuni katika Kliniki ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Kawe.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma ya upimaji na matibabu ya moyo bila malipo itakayotolewa kwa wasanii.
Dkt. Kisenge alisema kutokana na tatizo la magonjwa ya moyo kuwa kubwa Taasisi hiyo imeona ishirikiane na wasanii katika kuhamasisha jamii ili kuona umuhimu wa kupima magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.
“Katika kufanikisha hili kutakuwa na zoezi la upimaji wa magonjwa ya moyo bila malipo kwa wasanii katika kliniki yetu ya Kawe kwa mwezi wa huu wa Desemba na Januari 2024 kila siku za Jumamosi na Jumapili”.
“Baada ya kumalizika kwa zoezi hili kutakuwa na utaratibu maalumu kwa wasanii ambao hawana bima za afya watakaokuja kutibiwa katika kliniki yetu watapata punguzo la gharama za matibabu”, alisema Dkt. Kisenge
Nae Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama ongea na Mwanao, Steve Mengele maarufu kama “Steve Nyerere,” amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuwapa wasanii wa filamu fursa ya kupima afya zao ili kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo magonjwa ya moyo.
Aidha, Steve Nyerere amewasihi Watanzania wote kupima afya zao mara kwa mara ili kufahamu hali ya afya na kuishi maisha yenye umakini, kwa kuzingatia ulaji unaofaa.
“Wasanii waache kuchezea suala la afya. Wajitokeze kwa wingi kujisajili kwenye mamlaka zilizokasimiwa, ikiwemo Bodi ya Filamu Nchini pamoja na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kwa ajili ya kutambulika na kupata huduma ya kupima afya bila gharama yoyote,” amesema Steve Nyerere.
Ameongeza kuwa juhudi hizo zinalenga kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi hata katika maeneo ya pembezoni
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Dkt. Kedmon Mapana aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuona umuhimu wa kupima a fya za mioyo ya wasanii na kuwapa elimu ya jinsi ya kujiepusha na magonjwa hayo bila ya gharama zozote zile.
“BASATA tutasimamia zoezi hili la upimaji kwa wasanii wetu ili kila mmoja anufaike na upimaji huu kama mlivyosikia gharama za matibabu ya magonjwa ya moyo ni kubwa hivyo basi ni muhimu mkachukuwa hatua za kupima mapema kabla ya kusubiri kuugua”, alisisitiza Dkt. Mapana.
Naye Kaimu Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Gervas Kasiga alisema upimaji huo ni wa muhimu kwani utawapa hamasa wasanii ya kupima mioyo yao na kuchukuwa hatua baada ya kupata majibu ya vipimo hivyo.
“Ninawasihi mtumie vizuri fursa hii kwa kupima mioyo yenu na kupata elimu ya jinsi ya kujiepuka na magonjwa haya pia elimu mtakayoipata muitumie kuielimisha jamii inayowazunguka kwani uwezo wa kufanya hivyo mnao”, alisema Dkt. Gervas.