Taasisi ya Apps and Girls ya jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na Yas Tanzania imeendesha programu maalum ya mafunzo kwa wanafunzi wa sekondari kutoka shule tisa.
Mafunzo hayo yanalenga kuwainua wasichana kwa kuwapatia ujuzi wa vitendo katika masomo ya sayansi na ubunifu wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Carolyne Ekyarisiima, alisema mpango huo unalenga kuondoa tofauti ya kijinsia katika masomo ya sayansi na kuwajengea wasichana uwezo wa kujiajiri.
"Tunatoa mafunzo haya kuanzia ngazi ya shule za sekondari hadi kwa wale walio nje ya mfumo rasmi wa elimu. Wanajifunza kutengeneza roboti, kuelewa akili bandia, na kupata ujuzi wa ujasiriamali," alisema Carolyne.
Aliongeza kuwa programu hiyo pia ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono sera ya serikali ya kuongeza ushiriki wa wasichana katika masomo ya sayansi.
"Kila baada ya programu, wanafunzi hushindana kuunda miradi ya kiteknolojia, ambapo washindi hupewa zawadi ili kuwahamasisha zaidi," alibainisha.
Kwa upande wake, Meneja wa Mahusiano ya Nje wa Yas Tanzania, Rukia Mtingwa, alisema taasisi yao imeungana na Apps and Girls kusaidia kuhamasisha wasichana kuchukua masomo ya sayansi kutokana na uwiano mdogo wa kijinsia katika nyanja hiyo.