Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile ( wa sita toka kushoto mbele) katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali wakiwemo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) na Wakurugenzi wa Bodi hiyo, Mkurugenzi wa Mtendaji TASHICO, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Wabunge wa Mkoa wa Mwanza na Viongozi wa dini katika hafla ya uzinduzi wa jina na nembo ya TASHICO jijini Mwanza.
Waziri wa uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa (kushoto) akimsalimia Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Meli Tanzania
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Wakati Taifa likipanga kusherekea uhuru wa Tanganyika Desemba 9, Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) inaishukuru serikali ya awamu ya sita chini wa Uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa kwenye ujenzi wa meli ikisema utaendelea kuongeza biashara ya ndani na nchi Jirani.
Akiongea jijini Mwanza jana, Mkurugenzi Mkuu wa TASHICO Eric Hamissi amesema kuwa uwekezaji huu unaofanywa na Serikali kwa TASHICO katika ujenzi wa meli za mizigo utawezesha Tanzania kuimarisha biashara na nchi jirani kama Uganda, Kenya, Zambia, Burundi, DRC na Malawi, jambo ambalo litapanua soko kwa bidhaa za ndani na kuleta fedha za kigeni.
Alisema kuwa usafiri wa maji ni wa gharama nafuu ukilinganisha na usafiri wa barabara au anga kwani mizigo inayotoka bandari ya Dar es Salaam kuelekea Uganda kwa njia ya barabara hutumia muda mrefu kuliko ukitumia Ziwa Victoria kupitia Mwanza, mfano kutoka Bandari ya Dar es Salaam (Tanzania) hadi Kampala (Uganda) kwa barabara ni Kilometa 1,717 lakini kutoka Dar es Salaam hadi Kampala kupitia Ziwa Victoria ni Kilomita 1,470.
“Halikadhalika kwa Mizigo inayokwenda Kalemie, DRC ni rahisi kupita Ziwa Tanganyika kuliko kupita njia ya Barabara aidha upite Tunduma kisha Zambia Kilomita 1,922 au upitie Burundi kilomita 1,877. Ila kutoka Dar es Salaam kwenda Kalemie (DRC) kupitia Bandari ya Kigoma ni Kilomita 1,375,” alisema.
Aliongeza: ““Ningependa kutumia fursa hii kuwashukuru wadau wote ambao wamekuwa wameshirikiana nasi kwa njia mbalimbali katika safari yetu hadi sasa.”
Hamissi alitabanaisha kuwa mara tu baada ya Uhuru, Shirika lilikuwa chini ya Uangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini Serikali iliendelea kutoa huduma ya usafiri kwa njia ya maji katika maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa kwa kutumia meli tatu (3) za MV. Victoria (1960) na M.V. Clarias (1961) katika Ziwa Victoria; na M.V. Liemba (1913) katika Ziwa Tanganyika.
“Hata hivyo, Serikali ilinunua meli mpya saba (7): Ziwa Victoria: M.V. Butiama, (1980), MT. Ukerewe (1983), M.V. Serengeti (1988), Ziwa Tanganyika: M.T. Sangara (1981), M.V. Mwongozo (1982) wakati kwenye Ziwa Nyasa ni M.V. Songea, M.V. Iringa,” alisema.
Alisema kuwa MSCL ilianzishwa chini ya Sheria ya Makampuni sura 212, tarehe 08 Disemba 1997 kutoka Shirika la Reli (TRC). Lakini rasmi MSCL ilianza kazi tarehe 01, Agosti, 1999 ikiwa na meli 14 na boti moja,
“Hadi mwaka 2015, Kampuni ilikuwa inamiliki meli 14 ambazo kati ya hizo Meli 9 zipo katika Ziwa Victoria, Meli 3 na Boti 1 katika Ziwa Tanganyika na Meli 2 katika Ziwa Nyasa,” alisema.
Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa kwakuwa meli nyingi zilikuwepo kwa muda mrefu, hivyo zilichakaa na kupelekea nyingine kusimamishwa kutoa huduma kutokana ili kulinda usalama wa chombo na usalama wa maisha ya watu na mali zao ambapo mwaka 2017, Kampuni ilikuwa na meli tano tu zilizokuwa zinatoa huduma; Ziwa Victoria kulikuwa na MV.Umoja, MV Clarias wakati Ziwa Tanganyika kulikuwa na MV Liemba, MT Sangara na kwenye Ziwa Nyasa kulibaki na MV Songea.
“Mwaka 2018, Serikali ilianza kutenga fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa minne katika Ziwa Victoria na Mwaka 2022, Serikali iliielekeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kukabidhi meli tatu (3) za MV. Mbeya II, MV. Njombe na MV. Ruvuma kwa MSCL ambazo hadi sasa meli hizo zinaendelea kutoa huduma katika Ziwa Nyasa,” alisema.
AWAMU YA KWANZA YA MIRADI (2018 – 2023)
Alisema kuwa awamu hiyo ya kwanza ilihusisha miradi minne mojawapo ikiwa ni ujenzi wa Meli mpya ya MV Mwanza “Hapa Kazi Tu”, yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria, wakati tulifanya ujenzi wa Chelezo - ambayo inatumika kama kitanda cha meli kabla haijashushwa katika maji wakati ikiundwa. na meli ya MV. Mwanza iliundwa kwenye Chelezo hii,
“Kwenye awamu hii tulifanya ukarabati wa Meli za MV Victoria – Iliitwa New Victoria Hapa Kazi Tu ambayo inasafiri kutoka Mwanza Kwenda Bukoba kupitia Kemondo na ilianza kutoa huduma mwaka 2020 pamoja na kulifanyika ukarabati wa MV Butiama – iliitwa New Butiama Hapa Kazi Tu inasafiri kila siku kutoka Mwanza kwenda Nansio, kisiwa cha Ukerewe,” alisema.