Na Mwandishi wetu, Mwanza
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa matenki matano ya usambazaji maji, ulazaji wa mabomba makuu ya usambazaji maji pamoja na vituo viwili vya kusukuma maji (pump house) kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa Jiji la Mwanza na viunga vyake .
Mradi huo unatarajiwa kunufaisha wakazi wa maeneo mbalimbali hasa waishio maeneo ya pembezoni na yale yenye miinuko. Aidha matenki hayo yatapokea maji kutoka kwenye chanzo kipya cha uzalishaji maji cha Butimba.
Mradi umefikia asilimia 35% za utekelezaji, ambapo Matenki yenye jumla ya ujazo wa Lita Milioni 31 yanajengwa katika maeneo ya Kagera (Lita Milioni 10), Kisesa (Lita Milioni 5), Fumagila (Lita Milioni 10), Nyamazobe (Lita Milioni 5) na Usagara (Lita Milioni 1) huku mtandao wa bomba kwa urefu wa KM 40.5 ukitarajiwa kulazwa kutoka maeneo ya Vituo vya kusukuma maji vinavyojengwa eneo la Sahwa na Butimba kwenda kwenye matenki hayo.
Hadi sasa mtandao wa bomba umelazwa kwa urefu wa KM 13.7 huku kazi zingine za ujenzi zikiendelea kutekelezwa kwa kasi. Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2026 wakati baadhi ya kazi zikitarajiwa kukamilika mapema mwezi Machi 2026 ikiwemo ulazaji wa bomba la kupeleka maji tenki la Kisesa ambalo tayari ujenzi wake umekamilika.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wadau wa maendeleo kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (Agence Francaise de Développement - AFD) ukitarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi 450,000 wa Jiji la Mwanza na viunga vyake.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Waisa Werema, ambaye eneo lake limepitiwa na mradi huo, ameeleza kuridhishwa kwake na hatua kubwa ya maendeleo ilivyosaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa huduma ya maji kwa wananchi.
Aidha, ametoa pongezi kwa serikali na kwa Mkurugenzi wa MWAUWASA, Neli Msuya, kwa ushirikiano na viongozi wa mitaa katika kutatua changamoto zinapojitokeza mara moja.


