📍Dar es Salaam,
Waziri wa Madini na Uchumi wa Buluu wa Kenya, Mhe. Ali Hassan Joho, ametoa wito kwa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kushirikiana kwa karibu katika kuongeza thamani ya madini yanayopatikana ndani ya ukanda huo.
Waziri Joho alitoa kauli hiyo leo Novemba 20, 2024, akiwa Mgeni Rasmi katika Hafla ya Usiku wa Madini iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
“Tunapaswa kushirikiana kuhakikisha madini yanayotokana na nchi zetu hayauzwi yakiwa ghafi, bali yanaongezewa thamani kabla ya kuingia kwenye masoko ya kimataifa, hii ni fursa kubwa kwetu” amesema Joho.
Amesema kuwa, kutokana na uwepo wa rasilimali za madini katika ukanda wa Afrika Mashariki, matamanio yake ni kuona siku moja wanapatikana mabilionea wazawa wwanaotokanana shughuli za uchimbaji, usafishaji pamoja na biashara ya madini.
Aidha, Mhe. Joho amesisitiza kuwa, kama Kenya wameona umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania 2024 kwa kuwa wamepata nafasi ya kujifunza mbinu bora za kuboresha Sekta ya Madini kupitia mijadala na mafanikio yaliyoanisha kupitia mijadala inayoendelea.
Mhe. Joho amebainisha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika Sekta ya Madini, hasa kupitia maboresho ya Sheria na Sera za Madini na kuongeza kuwa “Hatua hizi zimebadili kabisa mwelekeo wa sekta hii hapa Tanzania na zinaleta fursa za kutengeneza matajiri wakubwa kupitia rasilimali zetu,” ameongeza Joho.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini wa Tanzania, Mheshimiwa Anthony Mavunde, alisisitiza kuwa Tanzania imejidhihirisha kuwa nguzo ya sekta ya madini katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tanzania ni powerhouse ya sekta ya madini. Uwekezaji wa kimkakati katika kuongeza thamani ya madini utaleta manufaa makubwa kwa uchumi wetu na jamii zetu kwa ujumla,” amesema Mavunde.
Ametaja manufaa hayo kuwa ni pamoja na Kuongeza Mapato ya Serikali kupitia kodi na ada za biashara zinazotokana na bidhaa zilizoongezewa thamani ni kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya kuongezewa thamani madini.
Waziri Mavunde ameongeza manufaa mengine kuwa kulinda na kuongeza ajira kwa wazawa, kuimarisha Sekta ya Viwanda kwa kuchochea ukuaji wa viwanda vya ndani, kukuza uchumi wa ndani kwa kuongeza mzunguko wa fedha ndani ya nchi sambamba na kuboresha biashara ya kimataifa kwa kuingia masoko ya kimataifa na bei za juu.
*Uganda Yasifu Jitihada za Tanzania*
Waziri wa Nchi anayeshughulikia Madini kutoka Uganda, Mhe. Phiona Nyamutoro, amesifu mafanikio ya Tanzania katika sekta ya madini, hasa katika ukusanyaji wa mapato, mpango wa kuongeza thamani ya madini, na usimamizi bora wa sekta hiyo.
“Tanzania imeonyesha mfano mzuri wa jinsi ya kusimamia sekta ya madini kwa tija, jambo ambalo linafaa kuigwa na nchi zote za Afrika Mashariki,” amesema Nyamutoro.
Hafla ya Usiku wa Madini huambatana na onesho la bidhaa za madini ya vito sambamba na kutoa tuzo kwa wadau waliofanya vizuri katika sekta ya madini nchini Tanzania.