Na Mwandishi Wetu, Geita
Wafanyakazi wa Mgodi wa Geita Gold Mine (GGM), kupitia Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na Kazi Nyingine (TAMICO), wameonesha dhamira ya kumiliki nyumba zao kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Haya yamebainika baada ya ujumbe kutoka NHC kufanya ziara katika mgodi huo mkoani Geita kwa lengo la kujadiliana na wafanyakazi kuhusu fursa za umiliki wa nyumba kupitia miradi ya shirika hilo.
Katika mazungumzo na uongozi wa GGM na TAMICO, wafanyakazi hao wameonesha utayari wa kununua nyumba katika maeneo mbalimbali nchini, wakizingatia NHC inatekeleza miradi mikubwa kama Samia Housing Scheme (SHC), Seven Eleven (7/11) Kawe, Morocco Square, na Medeli Phase III inayokuja hivi karibuni pamoja na Iyumbu Satellite Center. Wamesema wanathamini juhudi za NHC katika kujenga nyumba bora na wameeleza nia ya kununua nyumba katika miradi hiyo.
Pia, eneo la Bombambili, Geita lina miradi ya NHC ambapo baadhi ya wafanyakazi wameonesha utayari wa kununua nyumba. Wafanyakazi hao wamesema wako tayari kuwekeza katika maeneo ambayo yataendana na mahitaji yao binafsi na familia zao.
Katika hatua nyingine, wafanyakazi wa GGM wamependekeza uwezekano wa NHC kujenga nyumba 300 kwa ajili ya wafanyakazi wao katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwezesha wafanyakazi kumiliki nyumba zao. Pendekezo hili limeonesha hamasa ya wafanyakazi hao kuwa na makazi bora na ya kudumu kupitia ushirikiano na NHC.
Mwisho, wafanyakazi hao wameeleza kuridhishwa na ujio wa NHC mgodini hapo, kwani wengi wao hawakuwa na taarifa kamili kuhusu fursa za kupata nyumba kupitia shirika hilo. Sasa wamepata mwanga na wanatarajia kuanza safari ya kumiliki nyumba bora kupitia NHC.
Shirika la Nyumba la Taifa litaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kutekeleza miradi ya nyumba katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuboresha hali ya makazi.