Na Lilian Ekonga
Ujenzi wa Bandari ya kwanza ya uvuvi nchini Tanzania, Kilwa Masoko, iliyoko kwenye pwani ya Bahari ya Hindi katika mkoa wa Lindi, uko karibu kukamilika, ikiwa tayari imefikia asilimia 70.
Mradi huu ni hatua muhimu katika mkakati wa Tanzania wa kukuza sekta ya uvuvi wa bahari kuu na kuboresha maisha ya maelfu ya wavuvi.
Mradi huu, ambao unagharimu TSh 289.5 bilioni, unatarajiwa kutengeneza ajira 30,000 na unatarajiwa kuwa kamili ifikapo Januari mwakani.
Mara baada ya kukamilika, bandari hii itakuwa na uwezo wa kuchakata tani 60,000 za samaki kila mwaka, hatua muhimu katika jitihada za Tanzania za kuongeza uwezo wake wa kunufaika na soko lenye faida la uvuvi wa bahari kuu.
Mojawapo ya vipengele muhimu vya mradi huu ni kituo cha kuchakata samaki, ambacho kina lengo la kuwawezesha wavuvi wa ndani.
Wavuvi watawezeshwa kuongeza mavuno yao kutoka kilo 1 hadi kilo 100 kwa siku. Ongezeko hili litaongeza faida na kuboresha hali zao za kiuchumi.
Aidha, wanawake wanaoshiriki katika sekta hii wanatarajiwa kuona fursa zaidi katika kilimo cha mwani, huku uzalishaji ukitarajiwa kuongezeka kutoka tani 4,000 hadi tani 10,000 kwa mwaka, kulingana na taarifa za Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Mkurugenzi wa Miundombinu na Maendeleo katika Wizara hiyo, Bw George Kwandu, alisema kuwa kwa sasa Tanzania haijafaidika kikamilifu na uvuvi wa bahari kuu kwa sababu sehemu kubwa ya samaki huvuliwa na meli kubwa za kigeni au kutupwa kwa kukosa vifaa vya usafirishaji.
Bandari hii mpya itasaidia kutatua changamoto hizo, kuruhusu samaki ambao uvuaji wake hawajafungwa kwenye mikataba wa aina yeyote kuletwa Kilwa Masoko, ambapo watachakatwa na kuuzwa kwa wafanyabiashara, hivyo kuunda mnyororo wa usambazaji wenye ufanisi na faida zaidi.
"Bandari hii ya uvuvi italeta mabadiliko makubwa katika sekta ya uvuvi nchini Tanzania. Itakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 1,800 za bidhaa za samaki kwa wakati mmoja na kuhudumia meli zenye urefu wa hadi mita 35," amesema Bw. Kwandu.
Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko inatarajiwa kuwa kitovu cha uvuvi wa bahari kuu, ikileta miundombinu muhimu itakayokuza sekta ya uvuvi nchini Tanzania na kusaidia jamii za ndani kuongeza uzalishaji wao wa kiuchumi.
Mwezi uliopita, wakati wa Mkutano wa 8 wa Mawaziri Wanaosimamia Bahari, Maji ya Ndani, na Uvuvi wa Shirika la Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, alisema kuwa wavuvi wadogo wanachangia kwa kiasi kikubwa sekta ya uvuvi nchini.
Amesema asilimia 95 ya wavuvi wa Tanzania wanafanya kazi kwa kiwango kidogo, wakichangia kwa kiasi kikubwa uchumi na usalama wa chakula.
Tanzania huzalisha tani 472,579 za samaki kwa mwaka, huku tani 429,168 zikivuliwa kutoka kwenye maji ya asili. Sekta hii inachangia Sh3.4 trilioni kwa mwaka, ikiwa na ukuaji wa asilimia 1.9 na kutoa ajira kwa watu 230,000 moja kwa moja.
Kukamilika kwa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko kunatarajiwa kuwa na athari kubwa katika kubadilisha sekta ya uvuvi nchini Tanzania. Bandari hii inalingana na juhudi za hivi karibuni za Tanzania kuboresha teknolojia ya uvuvi na kufikia masoko ya kimataifa, hasa kwa samaki aina ya jodari (tuna).
Serikali ya Tanzania, kupitia Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu, imesaini makubaliano na wamiliki wa meli za uvuvi na kupata ufadhili kutoka USAID kwa ajili ya kutekeleza mfumo wa ufuatiliaji wa kielektroniki kwenye maji ya bahari kuu. Mpango huu unalenga kusaidia Tanzania kunufaika na soko la faida la jodari nchini Marekani.
Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko ni sehemu ya ajenda pana ya maendeleo chini ya utawala wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayolenga kuwawezesha wanaoshiriki katika sekta za uzalishaji wa Tanzania.
Rais, ambaye alizindua ujenzi wa bandari hiyo mnamo Septemba 2023, anaona mradi huo kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa buluu nchini, kikileta ajira na kurahisisha mchakato wa kuongeza thamani kwa bidhaa za samaki.
Serikali ya Rais Samia imeongeza kwa kiasi kikubwa bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi hadi Sh 460.334 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/25, kutoka Sh 176 bilioni mwaka wa 2021/22 na Sh 66.8 bilioni pekee mwaka wa 2020/21. Uwekezaji huu unaonyesha dhamira ya serikali katika kuimarisha mabadiliko ya kiuchumi kwenye sekta ya mifugo na uvuvi nchini Tanzania.
Wakati wa uzinduzi wa Bandari ya Kilwa Masoko, Rais Hassan pia alitaja mipango ya kujenga bandari nyingine kama hiyo Bagamoyo ili kufaidika na ukanda mpana wa pwani wa Tanzania.
Alisema bandari ya Kilwa itafungua fursa sio tu kwa wavuvi, bali pia kwa wale wanaohusika katika mchakato wa kuongeza thamani, kama vile kilimo cha mwani na uchakataji wa samaki.
"Kama Kilwa haitapata mabadiliko makubwa baada ya mradi huu, tutahitaji kukaa chini na kutathmini tatizo liko wapi, kwa kuwa serikali inawekeza fedha nyingi kuwawezesha wananchi na kutatua changamoto zao," Rais alisema.
Pia alizungumzia mipango ya kuboresha uwanja wa ndege ili kuwezesha usafirishaji wa bidhaa za samaki kutoka Kilwa, kulingana na mafanikio ya bandari hiyo.
Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko unatarajiwa kuchukua miezi 36, ikiwemo miezi 24 ya ujenzi na mwaka mmoja wa usimamizi.