BALOZI CHANA: TANZANIA INA MKAKATI MADHUBUTI UTAKAOFANIKISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA



📌Atoa wito kwa Watanzania kuyaishi maono ya Rais Samia

Waziri wa Maliasili na Utalii,  Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali imeandaa mkakati madhubuti wa Nishati Safi ya Kupikia wenye lengo   kuwaondoa watanzania katika adha itokanayo na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia. 

Balozi Chana ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akihamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia programu ya PIKA KISASA inayoendeshwa na Wizara ya Nishati. 

Amesema kuwa  Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, hivyo Watanzania wana kila  sababu ya watanzania kutotumia kutumia nishati isiyo safi.

Amesema Mkakati huo wa nishati safi ya kupikia ni wa miaka kumi ambao unatoa muongozo wa kufikia lengo la asilimia 80 ya watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Kuhusu suala la utunzaji wa mazingira, amesema asilimia 48 ya eneo la Tanzania ni misitu hivyo matumizi ya nishati safi ya kupikia yatasaidia uhifadhi wa misitu ili kuwa na uhakika wa mvua.

“Watanzania tupo takribani milioni 61 tunaenda milioni 62, kwa idadi hii kubwa tuliyonayo tusipoachana na matumizi ya nishati isiyo safi tunaona namna gani tunaenda kuharibu mazingira yetu, hii misitu tunaihitaji hivyo nishati safi ya kupikia ni muhimu kwa ustawi wa mazingira. ” Amesema Chana

Ameongeza kuwa matumizi ya kuni na mkaa yamekuwa yakisababisha uharibifu mkubwa kwenye misitu na ndicho chanzo cha upatikanaji wa mvua zisizo tabirika. 

Aidha, ametoa wito kwa jamii kuishi kwenye maono ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuondokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia.
Previous Post Next Post