NBAA YAASWA KUENDELEA KUTANUA WIGO NA KUWA MFANO WA KUIGWA KATIKA NCHI ZA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI NA SADC


Na Humphrey Msechu, Dar es salaam

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, ameihimiza Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) kuendelea kupanua wigo wake na kuwa mfano wa kuigwa na nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kukuza sekta ya uhasibu nchini. Waziri Chande aliyasema hayo wakati akihutubia wahitimu 1,216 katika Mahafali ya 46 ya NBAA yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa APC Hotel, Bunju, jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba yake, Naibu Waziri alieleza kuwa idadi ya wahasibu wenye sifa nchini bado haitoshelezi mahitaji ya sekta ya umma, achilia mbali sekta binafsi. Alisisitiza kuwa NBAA ina jukumu la kuhakikisha wahitimu wake wanapata ujuzi wa hali ya juu ili waweze kuchangia kwa tija katika uchumi wa taifa. Aliwataka wahitimu kuanzisha makampuni binafsi na kufuata taratibu za kisheria, huku Serikali ikiahidi kuunga mkono jitihada zao kwa kuandaa mazingira rafiki ya biashara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno, alieleza mchango mkubwa wa Wizara ya Fedha kwa Bodi, hususan katika kutoa ushauri wa kitaalamu. Alisema kuwa bodi imekuwa ikifanya mapitio ya sera na sheria zake, ambapo mwaka 2024 walitumia sheria ndogo tatu kusimamia mambo ya msingi, ikiwa ni pamoja na watu wanaoomba au kukata rufaa.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NBAA, CPA Prof. Sylvia Temu, alitangaza mpango wa kuanzisha stashahada maalum kwa njia ya mtandao ili kuongeza fursa za mafunzo kwa wataalam wa uhasibu nchini. Alisisitiza kuwa uadilifu ni msingi muhimu katika taaluma ya uhasibu, akiwataka wahitimu kusimamia maadili na kufichua maovu pale yanapojitokeza.
Kati ya wahitimu 1,216, wanawake walikuwa 640 na wanaume 576. Hafla hiyo ilihitimishwa kwa wito wa viongozi wa NBAA kwa wahitimu kuhakikisha wanaongeza thamani katika usimamizi wa rasilimali za taifa na kutoa ushauri mzuri unaojenga taifa.
Previous Post Next Post