Na Humphrey Msechu, DAR ES SALAAM
CHEMBA ya wafanyabiashara wanawake Tanzania TWCC imesema itahakikisha inawaweezesha wanachama wake wanawake na vijana kuweza kuongeza ushiriki katika fursa za manunuzi ndani ya serikali na sekta binafsi zitakazowasaidia kujikwamua katika biashara.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC Mwajuma Hamza wakati wa warsha ya siku moja ya vijana na wanawake wafanyabiashara na kufafanua kuwa Twcc ina matarajio makubwa kutoka kwa wanawake na vijana katika kuhakikisha wanakuza na kuinua biashara nchini.
Mwajuma amefafanua kuwa Serikali imejipambanua na imejiweka wazi kwenye progamu ya manunuzi ya umma na kupata fursa zilizopo kwa kuwajengea uwezo vijana na wanawake.
Nao baadhi ya washiriki wa kongamano hilo wamesema kuwa kila mtu anapofanya vizuri katika biashara ni kutokana na ufanyaji wake wa kazi unapelekea kupata tenda za kutosha kutoka katika sekta za umma na binafsi na mwenyekiti wa Bunju Women Jacqueline Mkina ameishukuru TWCC kwa mafunzo wanayowapatia kuhusiana na tenda na pia kuwawezesha kufahamu wapi pa kuchukua mtaji kwenye mabenki itakayokusaidia kufanyakazi.