TANZANIA YAWANOA WATAALAMU WA HALI YA HEWA AFRIKA KUHUSU MATUMIZI YA RADA ZA HALI YA HEWA


26 Agosti 2024, Mwanza, Tanzania: 

Katika kuwajengea uwezo wataalamu wa hali ya hewa kutoka Taasisi za Hali ya Hewa barani Afrika, Kitengo cha Elimu na Mafunzo cha Shirika la Hali ya Hewa Duniani kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kinachoendeshwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wameandaa mafunzo mahsusi ya matumizi ya data na taarifa za Rada za Hali ya HewaMafunzo hayo yanafanyika katika Ukumbi wa Malaika,Mwanza, tarehe 26 hadi 30 Agosti 2024.


Akifungua rasmi mafunzo hayo, Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb); alieleza lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha zaidi uwezo wa wataalamu wa hali ya hewa na wataalam wengine husika kutoka baadhi ya Nchi za Afika Mashariki na Kusini mwa Afrika katika matumizi bora ya taarifa za Rada za hali ya hewa kwa ajili ya kuboresha utabiri wa hali ya hewa na utoaji wa tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa kwa jamii.

Aidha, alieleza kuwa mafunzo hayo yanaendana na utekelezaji wa mpango ulioasisiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa utoaji wa Tahadhari kwa Wote (Early Warning for All EW4ALL) ifikapo mwishoni mwa mwaka 2027, pamoja na Sera ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ya ubadilishanaji wa data za hali ya hewa Kimataifa (“WMO Unified Data Policy”). 

Mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa nchi wanachama wa WMO kanda ya Afrika (WMO RA1) katika kuongeza uwezo unaohitajika zaidi wa utoaji wa huduma za hali ya hewa na tahadhari kupitia taasisi za hali ya hewa za nchi husika kukabiliana na ongezeko la idadi na ukubwa wa matukio ya hali mbaya ya hewa katika muktadha wa mabadiliko ya hali ya hewa na hivyo kuchangia kuokoa maisha ya watu na mali zao.


Alisisitiza umuhimu wa kufanya uwekezaji wa miundo mbinu ya kisasa ya hali ya hewa kama vile rada, akifafanua kuwa Tanzania imekuwa kilelezo bora katika kufanya uwekezaji huo pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa hali ya hewa nchini, na hivyo kuchochea fursa ya kuandaa mafunzo hayo.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Mwakilishi wa kudumu wa WMO, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hew ana Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a, alieleza kuwa TMA imejiandaa vyema kupitia wataalamu wake katika kutoa mafunzo hayo “Wataalamu watakao toa mafunzo ni wabobezi, na kati yao wamepata mafunzo kutoka Marekani na Finland na vilevile ni wakufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam”. Alisema Dkt. Chang’a.

Kwa upande wake, Mwakilikishi kutoka WMO (Ofisi ya Mafunzo), Bi. Eunjin CHOI aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kufanikisha mafunzo hayo muhimu ya matumizi ya taarifa na data za rada za hali ya hewa. “Kupitia ushirikiano huu, kwa pamoja tunaweza kuendeleza malengo yetu ya kuboresha huduma za hali ya hewa, si tu kwa Tanzania bali duniani kote”. Alisisitiza Bi. Eunjin.


Tanzania inatoa mafunzo kwa wataalamu wa hali ya hewa kutoka baadhi ya nchi Wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kanda ya Afrika ambao ni Burundi, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Msumbiji, Malawi, Mauritius, Rwanda, Seychelles, Sudan Kusini, Uganda, Tanzania na Zambia.

Previous Post Next Post