NIRC YAPIGA MARUFUKU KUFANYA SHUGHULI ZA UFUGAJI AMA KUVUA SAMAKI SEHEMU ZA UMWAGILIAJI


Na Mwandishi Wetu

DODOMA:HAIRUHUSIWI kufuga, kuchunga ama kuvua samaki katika maeneo yaliyotengwa rasmi kwenye shughuli za kilimo cha umwagiliaji.

Ofisa Sheria Mwandamizi kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Amina Mweta amesema hayo katika maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea katika Uwanja wa Nzuguni Dodoma.

Amina amesema sheria inakataza hayo kwamba maeneo ambayo yametangazwa kuwa ni sehemu ya kilimo cha umwagiliaji hayapaswi kutumika kwa shughuli nyingine.

Amesema pia sheria kwa kutambua kuwa miundombinu ya umwagiliaji inapaswa kujengwa na kukarabatiwa, " Kifungu cha 52 kimeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji ambao utachangiwa na serikali kuu, wadau wa sekta ya umwagiliaji pamoja na vyama vya umwagiliaji.

"Hiyo sheria imebainisha kwamba wakulima wa umwagiliaji wanapaswa kuchangia ada ya huduma ya umwagiliaji kwa kila msimu watakaovuna kwa asilimia tano tu ya mapato ambayo wanayapata," amesema.

Awali amesema sheria ya Taifa ya Umwagiliaji imetoa majukumu kwa tume kuratibu, kusimamia na kuendeleza sekta ya umwagiliaji nchini.

Amesema majukumu mengine ya tume ni kusimamia na kusajili vyama vya wakulima wa umwagiliaji.
Previous Post Next Post