MCB Bank yafungua ofisi Geita


Na Mwandishi Wetu, Geita

KATIKA kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita za kutanua wigo wa sekta ya fedha nchini Benki ya Biashara ya Mwalimu (MCB) Agosti 16, 2024 imefungua ofisi mpya Mkoani Geita kwa lengo la kuhakikisha wanawafikia wananchi wote kwa kuwasogezea karibu huduma za kifedha na kurahisisha huduma za kibenki ili kuleta tija kwenye ukuaji wa uchumi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Kaimu katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Dkt. Elfas Msenya amesema Mkoa huo ni wakimkakati kutokana na kuwepo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi, hivyo ni fursa kwa mabenki mengine kuungana na Benki ya Biashara ya Mwalimu kufungua ofisi zao hapa ili kutoa nafasi kwa wananchi kupata uhakika wa huduma za kibenki jambo ambalo litachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya fedha katika mkoa wa Geita.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa MCB Richard Louis Makungwa amesema wamefungua ofisi mkoani Geita kwa kuwa mkoa huo una fursa kubwa hususani ya biashara na uchimbaji wa madini, hivyo wameahidi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kwa kutoa huduma bora zaidi katika kuvutia wateja wadogo wadogo na wawekezaji mbalimbali ili kuwasaidia kukua kifedha na kuendelea kutumia benki ya biashara ya Mwalimu kwa huduma nzuri zaidi.

“Tunajua Geita ni mji wa madini na sisi tumejiandaa kikamilifu kuhudumia kwa ubora zaidi wateja wote, hususan wale wa sekta ya madini.” amesema Richard Louis Makungwa

Naye, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania Mwl. Joseph Misalaba amesema, Tusiishie kwenye kufungua matawi tu, bali pia elimu inapaswa kutolewa kwa walimu na wananchi mpaka kwa wachimbaji wa madini ili waweze kufahamu fursa zilizopo na umuhimu wake.

Hivyo, Afisa Elimu Mkoa wa Geita Mwl. Anton Mtweve ameshauri na kusihi Chama cha Walimu kuendelea kutafuta njia za kuleta ushindani kwa kuvutia wateja wengi zaidi na kuongeza mitaji ili matawi kama haya yaendelee kusambaa hadi kwenye halmashauri zote.
Previous Post Next Post