SAFARI ZA TRENI YA UMEME DAR - MORO KUANZA IJUMAA WIKI HII


Na Lilian Ekonga Dar es salaam.


Shirika la Reli Tanzania (TRC) imezindua  kampeni ya uelewa kuhusu kuanza kwa  huduma za usafiri wa Treni katika kiwango Cha kimataifa (SGR) zitakazo anza mwisho wa mwezi wa Julai kutoka Dar es Salaam-Dodoma ambapo tayari shirika limechukua hatua kadhaa ikiwemo kuanza safari zake tarehe 14 juni mwaka huu.

Hayo yalisemwa leo  Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Shirika hilo Masanja Kadogosa wakati akizungumza katika Hafla ya Uzinduzi wa kampeni ya uelewa kuhusu kuanza kwa huduma za usafiri wa Treni katika Reli ya kiwango cha kimataifa iliyoenda sambamba na kaulimbiu isemayo 'Twende tukapande Treni yetu, tuitunze, tuithamini'.


Amesema  kuanza kwa safari hiyo mwezi Juni itapelekea kuweza kugundua changamoto mapema za kwenye Reli hiyo na kuweza kuzitatua kwa wakati.

"Shirika litaanza kutoa huduma za awali za usafiri wa Treni katika Reli ya kiwango Cha kimataifa (SGR) kwa Dar es Salaam - Morogoro ifikapo tarehe 14 Juni 2024, kuanza kwa safari za Treni Dar es Salaam - Morogoro ni sehemu ya kuendelea kujifunza kwa kuwa teknolojia hiyo mpya nchini na kujiridhisha kwa mifumo mbalimbali ya uendeshaji huduma za usafiri wa Treni kabla ya kuanza rasmi safari ya kutoka Dar es Salaam - Dodoma ifikapo tarehe 25 Juali 2024"


Pia aliwataka wanachi waendelee kushirikiana katika kutunza miundombinu ya Reli hiyo kwani ni Mali ya watanzania na imejengwa kwa fedha za walipakodi wa Tanzania kwa kutumia huduma za TRC ili kuongeza pato la Taifa.

Aidha amesema ndani ya Reli hiyo kutakua na ulinzi wa kutosha kwa Reli yenyewe, abiria na mizigo kwa ujumla.

"Jambo hili ni muhimu sana kwa maana ya usalama wa Reli yetu,  usalama wa abiria na mizigo, kwani ukiacha kuwa na CCTV Camera tutakua na watu ambao watakuwa wanaangalia kile kinachoendelea kwenye treni yetu kwa masaa 24, pia uwepo wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ambapo tutakua  na maaskari kwenye Treni ambao watasafiri nasi mwanzo hadi mwisho"


"Kwenye miundombinu, pamoja na kufanya doria, stesheni zetu zote zinavituo vya polisi na tunaimani kuwa kutakua na utaratibu wa kuwepo na maaskari huko njiani, pia Askari watafanya doria, tutakua na walinzi watakuwa wanafanya kazi masaa 24"

Kadhalika Kadogosa alisema Abiria wanaweza kukata tiketi kwa njia ya mtandao au kupitia madirisha ya kukatia tiketi ndani ya stesheni ambapo kupitia njia ya mtandao abiria atatakiwa kukata tiketi wiki Moja au siku 3 kabla ya safari ili kuepukana na msongamano.


Kuhusu nauli Kadogosa amesema tayari LATRA wameshatangaza nauli na hivyo wateja wawe tayari kwa safari.

"LATRA wametangaza nauli za daraja la kawaida, lakini tutakua na Treni za aina tatu Terni ya kawaida itakayosimama Kila sehemu, tutakua na Treni za Moja kwa moja (Express) na Treni mchongoko"

Kwa upande wake Mkurugenzi  Mkuu wa Benki ya Biashara (TCB) Adam Mihayo alisema katika safari hizo za Reli ya SGR, TCB wameshirikiana na TRC katika kukusanya mapato katika vituo vya kukatia tiketi.


Pia Mihayo amesema Benki ya TCB  wameshirikiana na TRC kwa kufanikisha kuleta vichwa vya Treni na mabehewa kutoka Ujerumani.

"Ushirikiano wetu na Reli ya Tanzania unaakisi dhamira yetu ya pamoja ya kuelewa mahitaji ya watanzania na kuchangia katika ukuaji wa amaendeleo ya kiuchumi na mafanikio ya Taifa letu" 

"TCB tutaendelea kushirikiana na shirika la Reli Tanzania ili kuhakikisha matarajio ya Mhe. Rais katika mradi huu yanaweza kutimia" Alisisitiza
Previous Post Next Post