TMA yatoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa kipindi cha Juni - Agosti 2024


Na Mwandishi Wetu,

Katika kipindi cha msimu wa Kipupwe, 2024, hali ya joto la bahari katika ukanda wa tropiki ya kati ya bahari ya Pasifiki inatarajiwa kuwa ya wastani hadi chini ya wastani, ikiashiria kuelekea hali ya La Niña hasa mwisho wa msimu. Hali hii inatarajiwa kuwa na mchango hafifu katika mifumo ya mvua hapa nchini.

Kwa upande wa Bahari ya Hindi, joto la bahari la juu ya wastani linatarajiwa kuendelea kuwepo katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi (pwani ya Afrika Mashariki) ikilinganishwa na joto la Bahari upande wa mashariki mwa Bahari ya Hindi (Pwani ya Indonesia). Hali hii inatarajiwa kuimarisha mifumo inayosababisha mvua katika maeneo ya ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi na maeneo jirani. 

Hata hivyo Tahadhari za kiafya zinapaswa kuchukuliwe ili kulinda jamii dhidi ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na baridi na vumbi. Kutokana na hali ya ukavu inayotarajiwa katika maeneo mengi katika kipindi hicho, maji na malisho yanapaswa kutumika kwa uangalifu ili kupunguza athari zinazotarajiwa.

Aidha, wakulima wanashauriwa kulima mbogamboga na mazao ya mizizi kama vile viazi katika maeneo oevu na pia katika maeneo yanayotarajiwa kupata vipindi vya mvua katika kipindi hiki cha msimu wa Kipupwe. Hata hivyo, sekta za ujenzi, madini na uchukuzi zinaweza kunufaika kutokana na hali ya hewa inayotarajiwa.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa mrejesho hivyo Watumiaji wa taarifa za utabiri wanashauriwa pia kufuatilia na kuzingatia utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi pamoja na tahadhari za hali mbaya ya hewa kama zinavyotolewa na TMA.
Previous Post Next Post