TPA YASIMIKA MITAMBO YA KISASA YAKUPIMIA UJAZO WA MAFUTA NCHINI


Na Humphrey Msechu, Dar

Mitambo ya kisasa ya kupima ujazo wa mafuta ya aina zote yanayoingia nchini Tanzania (Flow Meters) ambayo imesimikwa katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara inatajwa kuinufaisha Serikali pamoja na wadau wa sekta ya mafuta.


Mitambo hiyo iliyosimikwa kwa awamu tatu na Serikali chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ina lengo la kupata takwimu sahihi za mafuta, yakiwemo ya kula, taa, ndege, petroli, dizeli, ya vilainishi na mafuta mazito mara yanaposhushwa kutoka kwenye meli.

Mbali na hilo, lengo la mitambo ni kuifanya teknolojia kuwa sehemu muhimu ya upimaji wa ujazo wa mafuta badala ya utashi, hivyo kupunguza makosa ya kibinadamu kama anavyobainisha na Mhandisi wa Idara ya Mafuta wa TPA, Yona Malago.


Mhandisi Malago amesema hayo leo Jumanne, Aprili 16, 2024 wakati wa ushiriki wa kuhakiki wa mitambo hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam. Amesema awali vilikuwa vinatumika vipimo visivyostahiki vya Dip Sticking na UTI.

“Hii mitambo mipya ina faida, kwanza Serikali inapata kodi na tozo stahiki zinazotokana na uingizaji wa mafuta nchini kutokana na utambuzi sahihi wa kiwango cha mafuta,” ameeleza Malago.


Ametaja faida nyingine kuwa ni kuongezeka kwa shehena ya mafuta yanayoagizwa na nchi za jirani kupitia Bandari ya Dar es Salaam ambazo zitalipwa kodi stahiki.


Ameongeza mitambo hiyo ni shirikishi, kwani inahusisha taasisi za Serikali za wadau wa mafuta kama vile Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Wakala wa Vipimo (WMA), Mamlaka ya Maapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Ofisi ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).






Previous Post Next Post