TFRA YAFUNGIA MAGHALA YA MBOLE YA KAMPUNI YA YARA KWA KITENDO CHA KUTAKA KUUZA MBOLEA ILIYOISHA MUDA


Na Lilian Ekonga, 
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kimefungia maghala na kusimamisha mara moja biashara za mbolea kwa kampuni ya YARA Tanzania Ltd Kwa kitendo chake Cha kufunga upya mbolea iliyoisha muda wake kwenye vifungashio vipya ikiwa ni kinyume na sheria ya mbolea ya mwaka 2009.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Joel Laurent wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema mbolea iliyokwisha muda wake haipaswi kufungwa upya na kurudisha sokoni.

Aidha amesema hayo yamebainika baada ya Mamlaka hiyo kufanya oparesheni mbalimbali kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama Kwa mikoa mbalimbali ambapo Mkoani Tabora ilibaini kuwa Kampuni ya YARA Tanzania Ltd ikifunga mbolea iliyokwisha muda wake kwenye vifungashio vipya vikionyesha kuwa mbolea inafaa kutumika.

Ameongeza kuwa mbolea hiyo ilikuwa na jumla ya mifuko 16,889 ya kilogramu 5 sawa na Tani 90 yenye thamani ya Tshs Milioni 226,000,000 ikiwa ni kinyume na sheria ya mbolea namba 9 ya mwaka 2009.

Sambamba na hayo amesema katika muendelezo wa oparesheni hizo Mamlaka Kwa kushirikiana na Vyombo vya ulinzi na usalama vya Mkoani Songwe imebaini uwepo wa udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wakishirikiana na wakulima Kwa kujiandikisha na kutaja mashamba hewa na hivyo kuwauzia mbolea za ruzuku kinyume na utaratibu na waliohusika walikamatwa na kufikishwa kwenye Vyombo vya Sheria.

Hata hivyo ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara, wakulima na mtu yeyote atakayekutwa na hatia ya kufanya udanganyifu kwenye Mpango wa serikali wa kutoa mbolea za ruzuku kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Katika hatua Nyingine Mkurugenzi Laurent amesema upatikanaji wa mbolea hadi kufikia Disemba 31 ulikuwa Tani 797,871 sawa na asilimia 89 ya mahitaji ya mbolea kwa mwaka 2023/2024 ambayo ni Tani 848,884.

Amesema hadi kufikia Januari 31 mwaka 2024 kiasi cha Tani 447,603 kimeuzwa ndani ya nchi na kufanya kiasi kilichopo Kwa sasa kuwa Tani 414,227 sawa na asilimia 103 ya mahitaji ya Tani 401,281 zinazohitajika ili kukamilisha msimu.
Previous Post Next Post