WIZARA YA MADINI, TANESCO, FARU GRAPHITE WAJADILI CHANGAMOTO YA UMEME MRADI WA MAHENGE


Na Mwandishi Wetu,

Ujumbe wa Wizara ya Madini ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Msafiri Mbibo, umekutana na Uongozi wa Kampuni ya Faru Graphite inayotekeleza Mradi wa Mahenge Graphite pamoja na na Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) kwa lengo la kujadili changamoto ya nishati ya umeme inayokabili Mradi wa Mgodi wa Madini ya Kinywe Mahenge.

Kwa upande wa Kampuni ya Faru Graphite, ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Black Rock Mining na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Faru Graphite John de Vries, umewasilisha hoja kadhaa wakati wa kikao ikiwemo changamoto ya nishati ya umeme na miundombinu ya barabara ambako pande zote zimekubaliana kufanya kazi kwa pamoja kutatua changamoto hizo kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika kutoa huduma hizo.

Wajumbe wengine waliohudhuria kikao hicho kilichofanyika Leo Januari 29, 2024 katika ofisi za Wizara Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma ni pamoja na Afisa Mkuu wa Fedha wa Kampuni ya Black Rock Mining, Paul Sims, na Mshauri Mkuu wa Masuala ya Biashara wa Kampuni ya Faru Graphite, Raphael Msoffe, Wataalam wa Wizara ya Madini wawakilishi kutoka Tanesco, Tanroads, na Tume ya Madini.

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu Mbibo amesisitiza kuwa azma ya Wizara ya Madini ni kuhakikisha inatatua changamoto inayosibu miradi yote ya uchimbaji wa madini nchini ili ianze shughuli za uchimbaji na kuendesha shughuli zao bila changamoto ikiwemo Mradi huo wa Mahenge Graphite.

Naye, Mwakilishi wa Shirika la Umeme Nchini Tanesco, John Mageni amesema kuwa Shirika hilo na Kampuni ya Faru Graphite ziko mbioni kusaini makubaliano ya kujenga kituo kidogo cha kupoozea umeme katika eneo la Mahenge kwa ajili ya kuhudumia mgodi huo ili uanze uzalishaji.

Mradi wa Mgodi wa Madini ya Kinywe wa Mahenge unatekelezwa na Kampuni ya Ubia ya Faru Graphite Corporation inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania inayomiliki hisa asilimia 16 huku asilimia 84 zikimilikiwa na Kampuni ya Black Rock kutoka nchini Australia.
Previous Post Next Post