Serikali imetoa Sh. bilioni 1.29 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi saba ya kitafiti nchini


Na Mwandishi Wetu, 

Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imetoa Sh. bilioni 1.29 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi saba ya kitafiti kutoka katika taasisi mbalimbali hapa nchini.
 
Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo na utoaji ufadhili huo kwa watafiti wanufaika wa miradi hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema fedha hizo zinatokana na tengeo katika bajeti kuu ya serikali pamoja na michango ya washirika wa maendeleo hususan Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Utafiti la Canada (IDRC) na Shirika la Maendeleo la Taifa la Norway (NORAD).
 

Amesema Serikali imeendelea kuongeza rasilimali fedha, kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuvutia wadau wengine ndani na nje ya nchi kuwekeza katika shughuli za utafiti na ubunifu nchini.
 
“Mazingira rafiki yameleta ambao umewezesha Serikali katika kipindi cha miaka mitano (2019-2022), kugharamia jumla ya miradi 49 ya utafiti, iliyojumuisha zaidi ya watafiti 235 kutoka Taasisi za Elimu ya Juu na zile za Utafiti na Maendeleo nchini,” amesema Prof Nombo
 

Ameongeza kuwa Taasisi 11 za Elimu ya Juu na Utafiti zimewezeshwa kukarabati na kununua vifaa vya maabara za utafiti na miundombinu mingine. Katika kipindi husika, kiasi cha Shilingi Bilioni 9.04 kimetumika katika kutekeleza matokeo hayo.
 
Akizungumzia matokeo ya utafiti utakaofanyika kupitia ufadhili uliotolewa Prof. Nombo amesema inatarajiwa kuimarisha ufaulu katika somo la hisabati kwa shule za msingi na sekondari, na kuongeza matumizi ya teknolojia zinazoibukia  hususan matumizi ya akili bandia katika kuchagiza maendeleo katika sekta za Kilimo na Uvuvi, Afya, Elimu, na Manunuzi serikalini.
 

"Nimefarijika kuona tafiti zimejikita katika maeneo muhimu ya jamii na yanashirikisha sekta husika, kipekee niwapongeze TAKUKURU ambao mmeshirikiana na vyuo kuingia katika ushindani na kushinda kupata ufadhili Hivyo nasisitiza watafiti kuhusisha wadau wa sekta husika na tafiti mnazofanya na kuzingatia vipaumbele vya tafiti kitaifa( National Reserch Agenda)", Amesema Nombo

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dkt. Amos Nungu amesema kupitia mashirikiano hayo yaliyopo, COSTECH imefanikiwa kuleta fedha za utafiti hapa nchini zenye thamani ya takribani TZS. 9 bilion kwa kipindi cha miaka minne. Fedha hizi zimepitia COSTECH kwenda kwa watafiti wetu, na zingine zimeenda moja kwa moja kwao.
 

Ametaja  baadhi ya maeneo yaliyonufaika na fedha hizi ni kuwa ni  Uanzishwaji wa Vigoda viwili vya utafiti katika chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika ya Nelson Mandela (NM-AIST) Arusha na Tathmini ya madhara ya COVID19 kupitia MUHAS, UDOM.
 
"Nitoe wito kwa taasisi za utafiti na vyuo vikuu kuleta Tungo zao (proposals) kwenye eneo la usalama wa chakula. Mwisho wa kuwasilisha ni tarehe 10.09.2023 na kiasi cha fedha za kitanzania shilingi milion 650 zitatumika kufadhili miradi ya utafiti itakayoshinda,”amesema Dkt. Nungu
 
Previous Post Next Post