SERIKALI IMEWAASA WANANCHI KUPIMA VINASABA VYA SELIMUNDU KABLA YA KUOANA

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua kongamano la kisayansi lililoandaliwa na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) jijini Dar es Salaam

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu aliyeshika jarida rasmi la Selimundu la Lancet akionesha kwa wanakongamano la kisayansi lililoandaliwa na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu akiwa na viongozi wa afya wakizindua jarida rasmi la Selimundu la Lancet jijini Dar es Salaam leo Julai 12, 2023 wakati wa kongamano la kisayansi lililoandaliwa na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) la kujadili mbinu ambazo zitaweza kupunguza tatizo la ugonjwa wa selimundu hapa nchini.

Na Mwandishi Wetu, Dar

SERIKALI imewaasa Wananchi kupima kupata vinasaba vya selimundu kabla ya kuoana ili kupunguza uwezekano wa kuzaliwa watoto wenye selimundu.

Imesema, mtu anaweza kuwa na vinasaba lakini si ugonjwa, kwani kama mume na mke wote wanavinasaba wakiwa pamoja uwezekano mkubwa wa asilimia mpaka Hamsini watoto watazaliwa na ugonjwa wa Selimundu lakini ikiwa mmoja anacho na mwingine hana basi kutapunguza uwezekano wa mtoto kuzaliwa na ugonjwa huo.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu ameyasema hayo leo Julai 12, 2023 jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza kwenye kongamano la kujadili mbinu ambazo zitaweza kupunguza tatizo la ugonjwa wa selimundu na uzinduzi wa jarida rasmi la Selimundu la Lancet liloandaliwa na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) la

Profesa Nagu amesema takribani watoto 11,000 hadi 14,000 wanazaliwa na ugonjwa wa selimundu kwa mwaka nchini na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya tano ulimwenguni kwa wagonjwa wengi, wa ugonjwa huo huku asilimia saba ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo ni kwa watoto chini ya miaka mitano.

Amesema kufuatia tatizo hilo serikali sasa imetoa muongozo wa matibabu ya selimundu nchini yanayoainisha nyanja zote kuanzia kupunguza tatizo hilo kwa kufanya utambuzi wa watoto wachanga na uhakika wa matibabu.

Muongozo huu unalenga kufanya utambuzi kwa watoto zaidi ya milioni mbili wanaozaliwa kila mwaka na kuhakikisha wanapata matibabu mapema ikiwemo chanjo, dawa za antibiotiki ili wasipate changamoto zitokanazo na selimundu. " amesema Profesa Nagu.

Aidha ameongeza kuwa, serikali itahakikisha inatoa huduma kwani wao wanajua namna bora ya kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo hayo, wanajua nini cha kufanya na kwa wakati gani hivyo, kuboresha matibabu ya watoto hao

Profesa Nagu ameongeza kuwa, serikali inafanya jitihada kuhakikisha inakabiliana na tatizo hilo ikiwemo kuwatambua watoto mapema katika hospitali zote saba ikiwemo ya Taifa, Kanda na Rufaa za Mikoa ili kuhakikisha matibabu ya watoto yanakuwa mazuri na bora," alieleza Profesa Nagu.

Kwa mujibu wa Profesa Nagu, watahakikisha dawa ambayo inabadilisha maisha ya watoto wenye selimundu ya Hydroxyurea inapatikana Tanzania kwani kama ikianza kutengenezwa hapa nchini basi itapunguza gharama na kuhakikisha inakuwepo muda wote badala ya kusubiri kuagiza kutoka nje ya nchi.

Amesema, sema kwa sasa Bohari kuu ya Dawa (MSD) inatoa dawa hiyo muda wote na kwamba serikali imetenga fedha kwa ajili ya kununua dawa hiyo ambayo ipo kwenye miongozo ya dawa na kusaidia hospitali na vituo vya afya kuagiza.

"Nipende kuwakumbusha waganga wafawidhi wa hospitali kuhakikisha dawa hii inapatikana kwenye vituo vyote vya afya kwani ipo na inapatikana wakati wote," alisema

Kuhusu upandikizaji uloto, Profesa Nagu alisema matibabu hayo hupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo hilo na hupatikana katika Hospitali za Benjamin Mkapa na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Amesema gharama za matibabu hayo ni makubwa kwa sababu inahitaji kufanyika vipimo vingi na vikubwa ambavyo hupatikana ndani na nje ya nchi.

"Katika bajeti ya mwaka 2023/24 serikali imetenga Sh bilioni tano kwa ajili ya upandikizaji na kwa sehemu kubwa itatumika kupandikiza uloto na figo," Amesema Profesa Nagu na kuongeza kusema kuwa wako tayari kufanya kazi na watafiti Kuhakikisha zinajibu matatizo ya Watanzania.

Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Apolinary Kamuhabwa amesema kuwa tafiti walizofanya zimechangia maboresho ya huduma za ugonjwa wa selimundu nchini ikiwemo upandikizaji wa uloto na kuanza kwa uchunguzi wa watoto wachanga.

"Katika kongamano hili tumewasilisha utafiti uliofanyika kuhusu ubadilishaji wa vinasaba vyenye selimundu kwa watoto wachanga ili kukabiliana na ugonjwa huo, Utafiti huo unalenga watoto wote watakaozaliwa na vinasaba vya selimundu ambapo wataondolewa vinasaba hivyo na kuwekewa vinasaba visivyo na ugonjwa kwenye damu zao hii itasaidia kuondoa kabisa ugonjwa huu," amesema Profesa Kamuhabwa.

Previous Post Next Post