DCEA NA UELIMISHAJI JUU YA MADHARA YA MIRUNGI KATA YA TAE WILAYANI SAME




Na mwandishi wetu

Kamishna Jenerali Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas Lyimo ametoa onyo kali kwa viongozi wa ngazi ya halmashauri watakaobanika kutochukua hatua stahiki kuhusiana na kilimo cha mirungi, na kusema kuwa watachukuliwa hatua za kisheria bila kujali nafasi zao.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema hayo jana katika operesheni ya uteketezaji wa mashamba ya mirungi katika Kata ya Tae iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Same katika mkoa wa Kilimanjaro.


Ametoa rai kwa viongozi wa halmashauri kuanzia Afisa Tarafa mpaka Mwenyekiti wa Kitongoji kuwa ni wajibu wao kuhakikisha wanadhibiti uhalifu wa kilimo na matumizi ya mirungi, pamoja na kutoa elimu kuhusu athari ya matumizi yake katika maeneo wanayosimamia kulingana na sheria za nchi.

“Ni wajibu wa kila kiongozi katika halmashauri kuhakikisha anadhibiti matumizi ya mirungi, ikiwa ni pamoja na kukomesha kilimo chake kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli mbadala wanazoweza kuzifanya ikiwemo kilimo cha mazao mengine yenye tija.


Pia, kwenda kwenye vyuo mbalimbali vya ufundi kupata ujuzi utakaowasaidia kwa namna moja au nyingine au kufanya biashara halali zitazokuwa chanzo cha mapato kwa ajili ya kujikimu na maisha wakiachana na biashara ya mirungi.”, Kamishna Jenarali Lyimo amesisitiza.

“Operesheni hii ni endelevu na tunatoa muda wa visiki vyote vilivyokatwa ving’olewe na mashamba yote ya mirungi yateketezwe mara moja, vinginevyo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa viongozi kuanzia tarafani mpaka kwenye vitongoji pamoja na wananchi wote wanaojishughulisha na kilimo haramu cha mirungi.”, Kamishna Jenerali Lyimo ameonya.





Akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi popote alipo kutojishughilisha na biashara ya mirungi na kutoa taarifa za kudhibiti uhalifu huo kwa mamlaka kwa kutumia namba maalum ambayo aliitoa kwa wananchi hao.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni ameagiza viongozi wa Kata ya Tae kusimamia zoezi la ung’oaji wa visiki vyote na kutekekeza mashamba yote ambayo hayajafikiwa yateketezwe ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.


Hukua akiwataka wananchi kutojihusisha tena na kilimo cha mirungi, pamoja na kuwahimiza kujishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula.

Akizungumzia athari za matumizi ya mirungi, Kamishna wa Kinga na Tiba DCEA, Dkt. Peter Mfisi ameeleza kuwa matumizi ya mirungi yanachochea uhalifu ikiwemo ugomvi na mauaji kwa sababu ya kuathiri uwezo wa kufikiri, jambo linalosababisha mtu kuchukua maamuzi yoyote pasipo kutafakari matokeo yake na kusema kuwa baadhi ya maeneo ambayo kilimo cha mirungi yamekithiri kuna changamoto kubwa wananchi wake kitabia.
Previous Post Next Post