Na Mwandishi Wetu, Tabora
Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) mkoa wa Tabora unaendelea na ujenzi wa barabara ya Kazilambwa Chagu yenye urefu wa km 36 ambao kwa sasa umefikia asilimia 89.62.
Barabara hiyo ya kiwango cha lami ambayo km 26 zipo Tabora na kipande cha km 10 kipo Kigoma inayotarajiwa kukamilika June 30 mwaka huu inajengwa kwa gharama ya Sh Bilioni 38.
Akizungumza katika eneo la mradi wilayani Kaliua Kaimu Meneja wa Tanroads mkoa wa Tabora Mhandisi Rwegosholwa Michael alisema mradi huo ambao unajulikana kama barabara ya Kaliua,Malagarasi,Ilunde inajengwa ulisainiwa Desemba 27 mwaka 2021 na mkandarasi Stecol Corparation aliyepo Dar es Salaam huku msimamizi wa mkandarasi huyo ni Tanroads Engineering Consulting Unit (TECU).
“Barabara hii ina urefu wa km 36 ambapo kati ya hizo km 26 zipo upande wa Tabora na km 16 zipo Kigoma inajengwa kwa gharama ya Sh Bilioni 38,kwa sasa ujenzi umeshafikia asilimia 89.62,”alisema Mhandisi Michael.
Alisema barabara hiyo ambayo mkataba unamtaka mkandarasi kujenga kwa miezi 33 na kati ya hiyo miezi 30 ni ya ujenzi na miezi mitatu kwa ajili ya maandalizi.
“Mpaka sasa mkandarasi ameshamaliza miezi 32,ameshafanya kazi mbalimbali ikiwemo kusafisha eneo la barabara km 33.8 kwa asilimia mia,kuondoa udongo wa juu km 33.1 asilimia 100,kuondoa tabaka la kwanza la barabara la G3 la km 31.63 kwa km 95.58,ujenzi wa layer (tabaka) la pili la lami km 21.5 sawa na asilimia 63.56,”alisema Mhandisi Michael.
Wakizungumzia barabara hiyo wakazi wa Ugansa wilayani Kaliua walisema kuwa barabara hiyo itafungua mikoa hiyo miwili ya Tabora na Kigoma.
“Kwa sasa shida ya usafiri inaanza kupunguza tulikuwa tunapata shida kutoka Kigoma kwa sababu yakutokuwa na barabara ya lami,hata hapa tulipo tunafanya biashara zetu vizuri kwa sababu ya barabara hii,”alisema Juma Hamisi ambaye ni dereva bodaboda.
Aliishukuru serikali kwakuendelea kuwajali wananchi wake wa mikoa hiyo kwakuwa walikuwa wakiamini hawawezi kufikiwa na maendeleo kwa haraka kutokana na umbali wa mikoa hiyo.
Alisema mbali na barabara hiyo Tanroads Tabora pia inahudumia mtandao wa barabara wa km 2,188.09 ambapo kati ya hizo km 967 ni za barabara kuu ambapo kati ya hizo km 1,158.01 ni za barabara za mkoa wakati km 62.99 ni barabara za wilaya.