Na Humphrey Msechu, Dar es Salaam
TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) na Chuo Kikuu cha Shanghai cha China wameingia Ushirikiano wa miaka mitatu ya kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa somo la hesabu ikiwemo mbinu wanazotumia kwa walimu pamoja na kufanya utafiti.
Akizungumza leo Machi 30,2023 jijini Dar es salaam, mara baada ya utiaji saini hati za makubaliano kati ya TET na Chuo hicho, Mkurugenzi Mkuu TET, Dkt. Aneth Komba amesema makubaliano hayo ya utafiti yatalenga kwenye somo la hesabu kutokana na changamoto za somo hilo kutokufanya vizuri kwa kipindi kirefu hivyo kuwa mwarobaini kwani Shangai ndiyo inaongoza kwa kutoa walimu na wanafunzi bora wa somo la hesabu Duniani.
Amesema kuwa baada ya makubaliano hayo wanatarajia kupata namna nzuri ya kufundisha hesabu ikiwemo kupata mbinu za kuweza kuwavutia wanafunzi kujifunza somo hilo.
Aidha amesema kuwa wamekubaliana baada ya mwaka mmoja kuongeza masomo mengine ambapo watafanya kwanza utafiti ili kujua wapi kunahitaji kushirikiana na chuo hicho kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo hayo.
"Kwa kuanza utafiti watakaoufanya utajikita zaidi kwenye somo la hesabu ikiwemo kufahamu changamoto na mbinu zipi bora kutumika katika mazingira ya Tanzania ambapo tafiti hizo zitajikita kwenye hatua ya shule za Msingi na Sekondari". Amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo ya Mitaala, Dkt Fika Mwakabunju amesema kuwa mradi huo utatoa motisha kwa walimu kutokana na kupewa njia sahihi za kuwafundisha wanafunzi hapa nchini.
Amesema kuwa kwa utafiti waliofanya wamegundua wenzetu wa Shangai wametuzidi kwenye masuala ya teknolojia hususani kwenye ufundishaji wa somo la hesabu.
Naye Mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Shanghai amesema kuwa wataendelea kushirikisha na Taasisi ya elimu Tanzania (TET), katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo mbalimbali hapa Nchini.