ACT WADAI UFAFANUZI FIDIA MABOMU YA MBAGALA


Na Mwandishi wetu, Dar es salaam

Chama cha ACT walezalenda kimemshauri Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi maalum wa Fungu la RAS wa Dar es Salaam kuona namna wa malipo ya fidia ya Wahanga wa Mabomu ya Mbagala yaliotokea aprili 29,2009 yaliyofanyika. 

Akizungumza na Waandishi wa Habari Leo jijin Dar es saalam Waziri Mkuu Kivuli wa ACT wazalendo, Dorothy Semu amesema katika ziara aliyoifanya kwa wakazi waliopatwa na ulemavu kutokana na athari za mabomu ya mbagala ameshuhudia makaazi yaliyoharibiwa ambayo hadi leo wamiliki wameshindwa kuyakarabati kutokana na kucheleweshewa fidia.

 "ACT Wazalendo kupitia Ofisi ya Waziri mkuu Kivuli ilifuatilia suala hilo kwa kuchambua taarifa mbalimbali (orodha ya waathirika, malipo, risiti za malipo, kiasi cha bajeti kilichotumika na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali-CAG) na baadaye kutembelea baadhi ya waathirika hao, tumeshangazwa sana kuona kwa zaidi ya miaka 14 tangu kutokea kwa milipuko hiyo kuna waathirika wapatao 1, 361 kutolipwa fidia zao" amesema Semu.

Ameongeza kuwa TAKUKURU ilipokea malalamiko ya uwepo wa rushwa na ilianza kufuatilia suala husika ni wakati sasa ikamilishe uchunguzi wake ili kubaini wahusika na mchakato mzima wa utoaji malipo kwa fidia kwa watu wasiohusika na mabomu ya Mbagala. 

Pia amesema taarifa mbalimbali za ushahidi ikiwepo majina 1,571 yaliyolipwa mwaka 2017 na 2018 ambayo si ya wakaazi wa kata 19 zilizokumbwa na kadhia ya mabomu zilifikishwa ofisi za TAKUKURU na waathirika waliopunjwa fidia.

Aidha ametoa wito kwa watumishi wa serikali kusikiliza madai ya wananchi na kutoa ufafanuzi stahiki huku akiomba Hatua stahiki zichukuliwe kwa wahusika wa Kitengo cha Maafa wanaotoa vitisho , kuwaapisha kinyume cha sheria, kuwajeruhi kama jitihada za kuwanyamazisha viongozi wa wahanga waliopunjwa fidia ili kuwavunja moyo wanapodai haki zao.
Previous Post Next Post