MAZINGIRA NI SISI NA VIZAZI VIJAVYO,TUTUNZE MISITU NA VYANZO VYA MAJI


Na Mwandishi Wetu

Hayo yamesemwa na Mkuu Wa Mkoa Wa iringa Mh. Halima Dendego Januari 16, 2023 alipokua katika Shamba la Miti la SaoHill kuzindua zoezi la ugawaji miche kwa wananchi wanaolizunguka shamba. 

Zoezi hilo limefanyika katika bustani ya Shamba Tarafa ya Kwanza Irundi ambapo wananchi na taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za kiserikali zimeweza kugawiwa miche hiyo.


Akizungumza na wananchi Mhe. Mkuu wa Mkoa Halima Dendego amewapongeza TFS kupitia Shamba la Miti SaoHill kwa zoezi hili la ugawaji wa miche kwa wananchi wanaolizunguka shamba kwani kwa kufanya hivi wanasidia katika kujenga uhusiano mzuri baina ya Shamba na wananchi.

"Nawapongeza sana TFS kupitia Shamba la SaoHill kwa zoezi hili mnalolifanya la kuwapatia wananchi miche na nawaomba msiishie hapa kwani miti inachangia katika ukuaji wa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla hivyo msisitishe zoezi hili" amesema Mh. Halima Dendego


Aidha aliendelea kuongea na wananchi na kuwaomba kuendelea kushirikiana na Shamba kwani wananchi ni wanaufaika wakubwa wa shamba hili na mapato yanayotokana na shamba yanawanufaisha wananchi wote wa Tanzania.

"Shamba hili linachangia kwa kiasi kikubwa mapato ya nchi yetu na hayo ndiyo yanayotumika katika kutatua changamoto nyingi za wananchi hivyo nawaomba wananchi muendelee kushirikiana vizuri na Shamba ili kuendelea kuhakikisha kuwa hifadhi zetu za misitu zinatuzwa vizuri kwani kwa kufanya hivyo tunakua tunatunza mazingira na vyanzo vyetu vya maji"Amesema Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa.

Aliendelea kwa kuelezea jinsi gani shamba lina umuhimu katika nchi yetu kwani asilimia 15 ya maji yanayoingia katika bwawa la Mwalimu Nyerere yanatoka katika vyanzo vya maji vinavyopatikana katika Shamba hili la Miti SaoHill hivyo anawaomba sana wanachi kuendelea kupanda miti katika maeneo yao na kutunza vyanzo vya maji.

Aidha alisikiliza pia changamoto wanazokumbana nazo wananchi katika utunzaji wa misitu na kuahidi kuwasaidia kutatua changamoto hizo ikiwemo kuwasaidia katika kupata vifaa ambavyo vitawasaidia kukabiliana na majanga ya moto katika misitu.

Amesema kuwa misitu iliyopo katika Mkoa wa Iringa imekua na faida kwa wananchi na taifa kwani inasaidia katika upatikanaji wa malighafi za viwanda na mapato kwa wananchi na taifa letu kwa ujumla.

Akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe.Saad Mtambule amesema kuwa wilaya inashirikiana vyema na Shamba la Miti SaoHill kwani wanajua na kutambua mchango wa Shamba hili katika Halmashauri zilizopo Wilayani Mufindi na Taifa kwa ujumla.

"Shamba la Miti SaoHill limekua na mchango mkubwa katika wilaya yetu kwani linasaidia upatikanaji wa malighafi za viwandani na kusaidia katika utunzaji wa mazingira yetu hivyo zoezi hili la ugawaji miche kwa wananchi linasaidia katika kujenga uhusiano bora baina ya wananchi na shamba"amesema Mkuu wa Wilaya

Akiwasilisha taarifa ya Shamba Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti SaoHill Ignas Lupala amesema kuwa shamba hutenga miche zaidi ya milioni moja kwa ajili ya kuigawa kwa jamii na Taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi zilizopo Wilayani Mufindi na maeneo jirani ili ipandwe katika maeneo yao kwa ajili ya kuhifadhi mazingira pamoja na kutumika kama chanzo cha kipato baada ya kuivuna na kuuza hata hivyo miche hiyo inayogawiwa kila mwaka ina thamani ya takribani TZS 300,000,000/=.

Aidha Mkuu wa Mkoa Halima Dendego alihitimisha zoezi hili kwa kugawa miche kwa wananchi, taasisi za serikali na zisizo za kiserikali na wananchi waliojitokeza kuomba miche hiyo
Previous Post Next Post