MAJAMBAZI SUGU WANNE WAKAMATWA NA JESHI LA POLISI DAR

 


Na Lilian Ekonga, Dar es salaam

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kuwakamata majambazi sugu wanne wanafahamia kwa majina,Athuman Yusuph Mbalilo  (50) Mkazi wa Kimara Temboni,  na Mpoki Raphael (41) mkazi wa Mbezi luis.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 9, 2023 jijini Dar es Salaam Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ACP Mulilo Jumanne Muliro amesema majambazi hao walikamatwa Januari 8, 2023 saa 6:30 mchana eneo la Mabibo Extrnal Kinondoni.

ACP Mulilo amesema kuwa wawili wanashikiliwa kwa tuhuma nzito  za kujihusisha na vitendo vya kihalifu vya  unyang’anyi wa kutumia silaha na kupora pesa  katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

“Ukamataji huo ulitokana na taarifa fiche ya kuwepo kwa kundi hilo la kihalifu ambalo lilionekana kuanza kufanya matukio mbalimbali ya uhalifu wa kutumia silaha kuanzia tarehe 01/01/ 2023 hadi tarehe 07/1/2023 katika Jiji la Dar es Salaam,” amesema ACP Muliro na kuongeza,

“Watuhumiwa hao wanne walikutana kupanga na kujiandaa eneo la kufanya uhalifu na walipobaini kuzingirwa na askari Polisi mmoja wao  alitoa bastola yake na kupiga risasi kuwashambulia askari, na katika mazingira hayo askari haraka walijihami na kuwajeruhi watuhumiwa wote wanne kwa risasi na kufanikiwa kuwakamata,”.

ACP Muliro ameeleza kwamba mahojiano ya awali na watuhumiwa hao na kumbukumbu za kihalifu za Polisi zimeonesha kuwa miongoni mwao waliwahi kukamatwa na kukaa kwenye mahabusu za Keko kwa tuhuma za mauaji na unyanganyi na walitoka 2017 na mmoja wao akakimbilia nchi jirani na alirudi 2022 na kushiriki matukio yakiwemo jaribio la uporaji eneo la Mtaa wa Tandamti  Kariakoo, kupora pesa huku wakitishia bunduki eneo la Kunduchi Mtongani, Goba walitishia silaha na kupora pesa, Keko, na Vikindu Wilaya ya Mkuranga pia walipora pesa.

“Watuhumiwa hao pia baada ya kukamatwa waliweza kuwaonesha askari bunduki aina ya AK 47 yenye namba za usajili UC 3889 1998 ikiwa na risasi 24 ndani ya Magazine, Bastola moja aina Star iliyofutwa namba ikiwa na Risasi nne (4) ndani ya magazini na zilikamatwa pia Pikipiki mbili aina ya Boxer nyeusi, MC 665 DMD na MC 475 DPH ambazoz zikitumiwa kwenda na kutoka kwenye maeneo ya matukio yaliyotajwa,” ameeleza ACP Muliro.

ACP Muliro ameongeza kuwa kutokana na majeraha waliyoyapata wakati askari wakijihami kwa risasi wahalifu hao walipelekwa hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu lakini hali zao sio nzuri.

Kwamba juhudi za kuwatafuta majambazi wengine ambao hawajakamatwa zinaendelea na lazima watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vingine vya kisheria. 

“Jeshi la Polisi linachukizwa sana na halitavumilia hata kidogo kuona wahalifu wakiwasumbua wananchi kwa vitendo vya kihalifu.Jeshi halitakuwa na huruma lakini litazingatia sheria kuwashughulikia kwa haraka sana kila atakaye jihusisha au kutenda vitendo  vya ovyo vya kihalifu,”.
Previous Post Next Post