ZAIDI YA VISHKWAMBI 6000 VYAKABIDHIWA KWA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO ZANZIBAR ILI KUONGEZA MOTISHA KWA WALIMU


Na mwandishi wetu,

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) leo Desemba 22, 2022 imetoa jumla ya vishkwambi 6,600 kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (WEMA) kwa ajili ya kugawa kwa walimu ili kuwapa motisha na kuvitumia kama vitendea kazi.

Makabidhiano hayo yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam kati ya Dkt. Francis Michael, Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Khamis Abdulla Said, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi na maafisa wa Wizara hizo.

Katika hafla hiyo Dkt. Michael amesema Kati ya vishkwambi 300,000 vilivyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya zoezi la Sensa ya watu na makazi iliamriwa vigawiwe katika sekta ya elimu ambapo vishkwambi 6,600 ni kwa ajili ya walimu Zanzibar.


"Huku Bara tuliwapa walimu vishkwambi kama motisha, yaani ni mali yao tukiamini watavitumia ipasavyo kama vitendea kazi muhimu na nyie mkifanya hivyo itakuwa ni vizuri kwa kuwa motisha kwa walimu ni kitu cha muhimu sana na ni agizo la Waziri Mkuu," amesema Dkt. Michael

Ameongeza kuwa ni matarajio ya Serikali kuwa vishkwambi hivyo vitakuwa chachu katika kuboresha mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji ili kuinua ubora wa elimu nchini.


Naye Katibu Mkuu Ali Khamis Juma ameshukuru kwa kupatiwa vishkwambi hivyo na kuahidi kuwapatia walengwa mara moja ili waanze kuvitumia kwa ajili ya kuwasaidia katika kazi ya ufundishaji wanafunzi.

"Nina furaha kubwa kupokea vishkwambi hivi na ninaamini vitaleta mapinduzi makubwa sana katika masuala ya Elimu kule Zanzibar. Nitahakikisha vinagawiwa kwa walimu kama ilivyoelekezwa ili matarajio ya Serikali yatimie," amesema Ali Khamis.


Kwa upande wake, Prof. Carolyne Nombo, Naibu Katibu Mkuu (WyEST) amesema katika maoni yanayopokelewa ya maboresho ya mitaala ni kuhusu uboreshaji somo la Tehama hivyo uwepo wa vishkwambi utakuwa ni msingi wa utekelezaji wa uimarishaji ufundishaji wa somo hilo.

"Tunaamini vishkwambi hivi vitaenda kuongeza ufanisi na kuleta matokeo chanya katika elimu ya Tanzania. Pia walimu wetu wafahamu kuwa Serikali zao zote mbili zinawajali kwa kutengeneza mazingira bora ya kufanyia kazi," ameongeza Prof. Nombo





Previous Post Next Post