KONGAMANO LA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KUFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM


Na Judith Chao. Dar es salaam.

Wizara ya Nishati imetangaza kuandaa kongamano la nishati safi ya kupikia yaani ‘(Clean Cooking Conference) ili kuchunguza vikwazo vinayodumaza matumizi ya nishati za kisasa za kupikia na kupendekeza mikakati ya kufanikisha upatikanaji wa nishati safi, za bei nafuu na endelevu nchini Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Waziri Nishati Mhe, January Makamba amesema Mkutano huo utafanyika tarehe 1 na 2 Novemba 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha watunga sera, wadau wa maendeleo, wajasiriamali, wawekezaji, wafadhili, wanataaluma na wananchi kwa ujumla.

Waziri Makamba afafanua kuwa Asilimia 72% ya nishati yote inayozalishwa nchini Tanzania inatumika majumbani na tungamotaka inachangia karibu asilimia 90 ya nishati yote inayotumika kwenye kaya. 

"Asilimia 63.5 ya kaya zote nchini hutumia kuni kupikia na asilimia 26.2 hutumia mkaa. Sehemu iliyobaki inajumuisha asilimia 5.1 ya kaya zinazotumia gesi za mitungi, asilimia 3 umeme, na asilima 2.2 ikiwa ni nishati nyingine"amesema Waziri Makamba

Pia Amesema Matumizi ya nishati ya tungamotaka kupikia yanahusishwa na madhara mbalimbali ya afya ikiwemo magonjwa ya mfumo wa upumuaji, uharibifu wa mimba na vifo vya watoto wachanga. 

"Takriban watu 33,000 hupoteza maisha kila mwaka nchini Tanzania kutokana na magonjwa yanayotokana na nishati chafu za kupikia zinazotumiwa majumbani ikiwemo kuni na mkaa huku Wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa wa janga hili"amesema Waziri January.

Aidha Waziri Makamba ameongeza kuwa Katika kongamano hilo wataalamu kutoka sekta za umma na binafsi watajadili masuala mbalimbali kuhusu hali ya kupika nchini Tanzania na kubadilishana uzoefu kuhusu nishati safi za kupikia, kutathmini sera, sheria, udhibiti, uwezeshaji wa kifedha na teknolojia ili kukabiliana na changamoto hizo.

Waziri amemaliza kuwa Tanzania kwa sasa ni moja ya nchi za chini kabisa duniani kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia tukiwa na kati ya 4-5% ya watu wanaitumia na Lengo letu likiwa ni kupandisha idadi hii hadi kufikia 80% katika miaka 10 ijayo.

Kwa upande wake Dkt Pauline Chale, Mtaalamu wa Magojwa ya kupumua kutoka Hospitali ya Muhimbili amesema wanatibu wagojwa walioathirika na matumizi ya kuni na mkaa huku matibabu yake yakichua muda mrefu na yanatumia rasilimali nyingi ambayo ingeweza kutumika kutibu wagonjwa wengine.
Previous Post Next Post