Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Wiebe De Boer akifungua warsha maalumu iliyoandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa wajili ya kuwajengea uwezo wahariri na waandishi wa habari kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.
Na Humphrey Msechu
Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Wiebe De Boer amesema vyombo vya habari vikiwa huru vinaweza kuwa mhimili wa nne wa utawala.
Balozi Boer ameyasema hayo leo Jumatano Oktoba 20, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akifungua warsha maalumu iliyoandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa wajili ya kuwajengea uwezo wahariri na waandishi wa habari kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.
Amesema uhuru wa vyombo vya habari ni muhimu kwa maendeleo ya taifa kwa sababu inaongeza uwazi na uzalishaji katika maeneo ya kazi.
Amewataka waandishi wa habari kushirikiana na wadau wengine katika kuhamasisha mazingira wezeshi ya uhuru wa habari hapa nchini.
"Katika majadiliano haya kuhusu Sheria za Habari, nafurahi kuona idadi nzuri ya wanawake, hili ni muhimu pia, ninatarajia wataongezeka zaidi," amesema Balozi Boer.
Awali, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile amesema mwamko wa uhamasishaji wa mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari umeongezeka na umetoa matokeo mazuri.
"Kuna mafanikio mengi sana katika kampeni ya kuhamasisha mabadiliko ya sheria hii, nikitaja yapo zaidi ya 20. Hii inatokana na msaada mnaotupatia," amesema Balile.
Miongoni mwa mafanikio hayo, amesema ni kufunguliwa kwa magazeti ya Tanzania Daima, Mseti, Mawio na MwanaHalisi ambayo yalikuwa yamefungiwa kuendesha shughuli zao.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa zamani wa TEF, Theophil Makunga amesema uhamasishaji wa marekebisho ya sheria umeongezeka kutokana na msaada unaitokewa na Ubalozi wa Uholanzi.
"Tumefikia kiwango hicho cha kuhamasisha marekebeisho ya sheria kwa sababu ya support mnayotupatia," amesema Makunga akimweleza Balozi Boer.