Na Humphrey Msechu
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema, serikali imekamilisha rasimu ya muswada wa Sheria ya Bima ya Afya, na imewasilisha rasimu ambayo imesomwa kwa mara ya kwanza katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, Waziri Ummy amesema Sheria ya Bima ya Afya kwa wote itaweka utaratibu wa kuchangia gharama za matibabu kabla ya kuugua ambapo kila mtu atapatiwa kadi baada ya kujiunga na bima ya afya.
Amesema utaratibu huo utawawezesha wananchi kuchangiana, ambapo anayeugua na kuhitaji matibabu atachangiwa gharama za matibabu na wale ambao watakuwa hawaumwi kwa kipindi husika.
Kwa mujibu wa Waziri huyo wa Afya, utaratibu huo unaondoa hali iliyopo sasa inayomlazimu mtu kubeba mzigo peke yake wa kulipa gharama kubwa za matibabu anapokuwa ameugua.
Amesema wakati wa utekelezaji wa sheria hiyo, wananchi watakuwa na uhuru wa kujiunga na Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya au kampuni binafsi zinazotoa huduma ya bima kadri kila mtu atakavyoona inafaa.
Hata hivyo Waziri Ummy amesema pamoja na kwamba kila mtu anatakiwa na sheria hiyo kujiunga na bima ya afya, serikali haikusudii kuitekeleza kwa kukamata watu ambao kwa kipindi fulani watakuwa hawajajiunga na bima ya afya.
Aidha, Waziri Ummy amesema serikali inatarajia kufungamanisha umiliki wa kadi ya bima ya afya na upatikanaji wa baadhi ya huduma za kijamii kama ambavyo baadhi ya huduma zilivyofungamanishwa na umiliki wa kadi au namba ya kitambulisho cha Taifa (NIDA).
Lengo la kufungamanisha umiliki wa kadi ya bima ya afya na baadhi ya huduma, ni kuepuka adhabu za kukamata na kushtakiwa mahakamni kwa watu wasio na kadi ya bima ya afya kwa kuwa kufanya hivyo hakutaiwezesha serikali kufikia lengo la kila mwananchi kupata huduma za afya.
Kwa upande mwingine, serikali imesema kufungamanishwa kwa baadhi ya huduma za kijamii kunatarajia kuweka msukumo kwa wananchi ili wachukue hatua za kujiunga na bima ya afya na kuepuka changamoto za kutokuwa na uhakika wa kupata huduma za afya wanapozihitaji kutokana na kikwazo cha fedha.