Yaeleza Utafiti wa Gesi ya Helium uko kwenye hatua nzuri
Na mwandishi wetu, Dodoma
Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa amekutana na Watendaji wa Kampuni ya Noble Helium Limited inayofanya shughuli za utafiti wa gesi ya helium nchini.
Kikao hicho kimelenga kupata taarifa kuhusu maendeleo ya shughuli za utafiti wa gesi ya helium zinazofanywa na kampuni hiyo katika Mikoa ya Rukwa, Songwe, Katavi na katika eneo la Ziwa Eyasi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Justyn Wood,
amesema shughuli za utafiti zinazofanywa na kampuni hiyo katika maeneo ya tafiti ziko kwenye hatua nzuri.
Mbali na kubainisha maendeleo ya utafiti huo, amesema zipo changomoto kadhaa ambazo kampuni hiyo inakabiliana nazo ikiwemo upatikanaji wa vibali vya utafiti na hivyo kuiomba Wizara kusaidia ili kuwezesha shughuli za mradi kutekelezwa kwa wakati uliopangwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini amewaeleza watendaji hao kuwa kutokana na umuhimu wa mradi huo kwa manufaa na maendeleo ya Taifa, Serikali itazifanyia kazi changamoto zinazoikabili kampuni hiyo ili kuwezesha kufikiwa kwa malengo ya mradi huo.