PROF. MKUMBO: WADAU WA HABARI WATAKIWA KUJIPANGA WATAKAPOITWA NA KAMATI KATIKA KUTETEA HOJA ZA MABADILIKO YA SHERIA YA HABARI



Na Humphrey Msechu,

Mbunge wa Ubungo (CCM), Profesa Kitila Mkumbo amewataka wadau wa habari kujipanga ili watakapokuja kwenye kamati husika waweze kutoa hoja zao kwanini wanataka baadhi ya vifungu katika Sheria ya Huduma za Habari 2016 viboreshwe.

“Unafahamu kwenye kamati ndio wadau wanapata nafasi ya kutoa hoja zao kwanini wanataka baadhi ya vipengele vifanyiwe marekebisho,” amesema Profesa Kitila

Naye Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota amesema hawezi kuzungumzia chochote hadi hapo watakapouona muswada wa marekebisho hayo.

“Siwezi kuzungumzia chochote kwasababu kwenye ratiba hauonyeshi kuwa utakuja. Ukija basi tutaangalia marekebisho gani yaliyopo na kuuchambua kama utaletwa katika kamati yetu,” amesema Chikota ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Mwandishi wa kujitegemea Moses Michael, amesema anamini wabunge hawatapitisha mambo yatayochangia kufifisha sekta ya habari

“Mimi nataka kuwepo na Baraza Huru la Habari ndani yake kuwa na bodi ya ithibati itakayokuwa na jukumu la kuidhinisha waandishi wa habari kuwasaidia katika masuala mbalimbali,” amesema

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema mpaka sasa hawajajua ni lini marekebisho hayo yatapelekwa bungeni ingawa wanaamini Serikali imeonyesha nia njema ya kufanya mabadiliko.

“Waziri wa Habari ndiye mwenye kujua lini watapeleka bungeni muswada lakini sisi wadau tumepewa fursa ya kutoa maoni yetu na tumeona dhamira njema ya Serikali hadi hivi sasa, tukiendelea hivi nadhani huko tuendako tutashirikiana vizuri kwa masilahi ya Taifa letu,” amesema

Naye Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, amenukuliwa na chombo kimoja cha habari akisema mchakato wa marekebisho hayo uko kwenye hatua nzuri hivyo kuwataka wadau wavute subira
Previous Post Next Post