Mhe. Mizengo Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu na mkewe Bibi. Tunu Pinda katikati wakiwa katika picha ya pamoja na watalii kutoka china na wanafunzi wa Shule ya Msingi Gifted Kids aliokutananao alipotembelea Kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam
Na Mwandishi wetu.
Waziri Mkuu wa Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda ameagiza Makumbusho ya Taifa la Tanzania kuendelea kutangaza vivutio vya Makumbusho na malikale kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mhe. Pinda aliyasema hayo alipotembelea Kijiji cha Makumbusho kilichopo Kijitonyama Jijini Dar es Salaam akiambatana na mkewe Bi Tunu Pinda.
Amesema Makumbusho ya Taifa inatakiwa kuendelea kuweka mikakati ya kutangaza vivutio vya Makumbusho na malikale ili kukuza utalii nchini.
“Tuendelee kuweka mikakati zaidi katika kuitangaza Makumbusho na vivutio vyake kwa lengo la kukuza Utalii na hasa kwa kizazi kilichopo na kijacho”. alisema Mhe. Pinda
Mhe. Pinda alipata nafasi ya kujua historia na tamaduni za Makabila 120 ya Tanzania kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho Bi Agnes Robert.
Akiwa Kijiji hapo alipata nafasi ya kukutana na watalii wengine kutokea nchini China ambao walikuja kutalii Kijiji cha Makumbusho na kujifunza historia ya Makabila ya Tanzania na teknolojia ya ujenzi wa nyumba za asili.
Mhe Pinda alifurahia kukutana na watalii hao kutoka China na kuzungumza nao kuhusu walichojifunza walipotembelea Kijiji cha Makumbusho.
Vile vile alipata nafasi ya kukutana na watoto wa shule ya msingi Gifted Kids, waliokuja kufanya utalii Kijijini hapo kujifunza utamaduni unaohifadhiwa hapo.
“Nimefurahia kuwaona watoto wadogo wakicheza ngoma za asili kwani hivi ndivyo inatakiwa maana watoto wanaona na kufanya kwa vitendo hivyo hawezi kusahau”. alisema Mhe. Pinda
Mwisho alipata nafasi ya kuwatembelea wajasiriamali waliopo Kijiji cha makumbusho na kutoa ushauri kwa uongozi wa Makumbusho ya Taifa kuangalie jinsi ya kutangaza kazi hizi za sanaa za mikono kwani ni moja ya kivutio kwa watalii.
' Makumbusho ya Taifa iangalie jinsi ya kutangazaa bidhaa hizi maana ni sehemu ya utalii' alisema Mhe. Pinda