Neville Meene mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), akizungumza katika Kipindi cha Front Page kinachorushwa na Radio +255 Global jijini Dar es Salaam.
Neville Meene mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), akiwa katika Kipindi cha Front Page kinachorushwa na Radio +255 Global jijini Dar es Salaam.
Na Humphrey Msechu
SHERIA ya habari ya mwaka 2016 ilianza kulalamikiwa kwa kipindi kirefu na wadau wa habari kwa kuwa haikuondoa mitego iliyowekwa na sheria ya mwaka 1979 na kuchangia kudumaa kwa vyombo vya habari nchini.
Hayo yamesemwa na Neville Meena ambaye ni mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), wakati akizungumza katika Kipindi cha Front Page kinachorushwa na Radio +255 Global jijini Dar es Salaam.
Meena amesema kuwa sheria hiyo ilianza kupigiwa kelele kwa muda mrefu na wadau wa habari ambapo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan iliona haja ya kukaa meza moja na wadau wa habari ili kuipatia ufumbuzi.
‘‘Hatua zilianza kuchukuliwa kwa serikali kuleta mapendekezo ya maeneo ya kurekebisha, lakini na sisi tuliongeza yetu ambayo wao walikuwa hawajaweka kwenye mapendekezo yao kwa kuwa mabadiliko hayo yalianzia kipengele cha 38.
“Sheria ya Habari ya Mwaka 1976, imefanya kazi kwa miaka 40, muda wote huo imetoa mwanya kwa mtu mmoja (waziri) kufungia chombo cha habari anapojisikia kufanya hivyo.
“Hata Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 ilipotungwa, imefuata mkondo huo huo wa kutoa mamlaka kwa mtu mmoja kuamua kufungia chombo cha habari ama la ingawa mamlaka hayo amepewa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Malelezo.Katika mabadiliko haya, tumeiomba serikali iondoe kipengele hicho,’’amesema Meena.
Mei 2,202 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alielekeza Sheria za Habari ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kubinya uhuru vya vyombo vya habari nchini zirekebishwe.
Rais Samia alitoa maelekezo hayo wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari
ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti’katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.
“Nimeelekeza Sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,”aliagiza Rais Samia