MBIBO: KAMPUNI ZA KITANZANIA ZIENDELEE KUWEZESHWA KUSHIRIKI KWENYE SEKTA YA MADINI



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo ameitaka Tume ya Madini kuendelea kuangalia namna ya kuziwezesha kampuni za kitanzania kwenye utoaji wa huduma kwenye shughuli za uchimbaji wa madini ili kampuni hizo ziwe na mchango kwenye ukuaji wa Sekta ya Madini.
 
Mbibo ameyasema hayo leo tarehe 22 Septemba, 2022 kwenye kikao chake na uongozi wa Tume ya Madini Makao Makuu jijini Dodoma kwa lengo la  kupata  taarifa ya utendaji kazi na  kutatua changamoto sambamba na kutoa maelekezo mbalimbali.
 
Amesema kuwa, pamoja na Tume ya Madini kuendelea kufanya kazi nzuri kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini, mikakati zaidi inahitajika kwenye eneo la ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini kwa kuhakikisha kampuni za kitanzania nyingi zaidi zinawezeshwa kwa kupewa mafunzo na kushiriki kwenye utoaji wa  huduma kwenye migodi ya madini na kuzalisha ajira kwa wananchi wanaozunguka migodi.
 


“Zipo kampuni za utoaji wa huduma mbalimbali ikiwemo vyakula, bima, ulinzi ambazo ninaamini zikiwekeza kwa wingi kwenye migodi ya madini zitaweza kuzalisha ajira kwa wananchi wanaoishi jirani na migodi hivyo kuongeza mzunguko wa fedha na uchumi wa maeneo yao kuendelea kukua huku Serikali ikiendelea kupata kodi,” amesema Mbibo.
 
Katika hatua nyingine, Mbibo ameitaka Tume ya Madini kuendelea kuongeza kasi kwenye ukusanyaji wa maduhuli ili kufikia lengo lililowekwa  na Serikali la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 822 kwa mwaka wa fedha 2022-2023
 


Aidha, amesisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto zinazojitokeza kwenye utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Madini na kuongeza kuwa milango ipo wazi kwa ajili ya kupokea mapendekezo mbalimbali kutoka Tume ya Madini yenye lengo la kuboresha utendaji wa Sekta ya Madini.
 
Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba sambamba na kumshukuru Naibu Katibu Mkuu kwa kutembelea Tume amesema kuwa mikakati mbalimbali imeendelea kuwekwa na uongozi wa Tume ya Madini kwenye uboreshaji  wa utendaji kazi hasa kwenye eneo la ukusanyaji wa maduhuli kwa kufanya vikao vya ndani hasa na maafisa madini wakazi wa mikoa.
 


Awali akisoma taarifa ya utendaji kazi wa Tume ya Madini kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, Mkurugenzi wa Huduma za Tume, William Mtinya amesema kuwa Tume kupitia Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa nchini imefanikiwa kuanzisha jumla ya Masoko ya Madini 42 na vituo vidogo vya ununuzi 78 nchini pamoja na kuboresha Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa.
 


Ameongeza kuwa Tume ya Madini imeweka mikakati ya uboreshaji wa utendaji kazi ikiwa ni pamoja na maboresho ya Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa na ununuzi wa magari mapya na vifaa vingine kama mkakati wa kuimarisha Sekta ya Madini.
 
 
 
 
Previous Post Next Post