Na Daniel Limbe,Biharamulo
BAADA ya Kampuni ya ununuzi wa Tumbaku nchini Japani (Japan Tobacco Incorparation) Kumhakikishia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,kuwa ipo tayali kwa msimu ujao kuja nchini kununua tumbaku kwa wakulima,baadhi ya wakulima zao hilo wilayani Biharamulo mkoani Kagera wamepokea kauli hiyo kwa shangwe huku wakionyesha matumaini mapya kwa zao hilo.
Waziri Mkuu yupo nchini Japan kumwakilisha rais Samia Suluhu Hassan, kwenye mazishi ya Waziri Mkuu mstaafu wa nchi hiyo,Shinzo Abe, anayetarajiwa kuzikwa kesho nchini humo,ambapo leo Majaliwa amefanikiwa kukutana na mtendaji mkuu wa Kampuni ya JTI, Masamichi Terabatake,ambaye ameahidi kununua kg 30,000,000 za tumbaku kutoka kwa wakulima Tanzania.
"Leo bodi ya wakurugenzi imetangaza uamuzi wa kununua kilo milioni 30 za tumbaku kutoka kilo milioni 14 ambazo ilinunua msimu uliopita...hii ni fursa kubwa kwa wakulima wetu kwani kiasi hicho ni zaidi ya uzalishaji wa zao letu nchini Tanzania...Kwahiyo wakulima sasa waongeze uzalishaji ili tufikie lengo hili"amesema Majaliwa.
Kutokana na kauli hiyo,Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,Leo Lushau,ameipongeza serikali kwa kuwatafutia wakulima wa tumbaku masoko ya uhakika nje ya nchi na kwamba hali hiyo itasaidia kuinua upya mwamko wa wakulima kupenda kilimo hicho ambacho tayali walikuwa wameanza kukata tamaa.
Amedai kuwa baadhi ya makampuni ya wazawa ya ununuzi wa Tumbaku yamekuwa yakiwakatisha tamaa wakulima ikiwa ni pamoja na kuikosesha mapato halmashauri yake, jambo linalochangia kuchelewa kukamilika kwa miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake Ofisa kilimo wa halmashauri hiyo,Bruno Ngawagala,amesema ujio wa Kampuni ya JIT ni neema kwa wakulima wa tumbaku wilayani Biharamulo kwa madai kuwa baadhi ya makampuni yamekuwa yakiingia sokoni pasipo kuwa na mtaji toshelevu kikidhi malipo ya wakulima.
Hatua hiyo imekuja huku baadhi ya wakulima wilayani humo wakiwa hawajui hatma ya fedha zao baada ya kukopwa na moja ya kampuni (jina tumelihifadhi) tangu msimu wa kilimo wa 2020/21 na kushindwa kuwalipa huku halmashauri ya wilaya hiyo nayo ikidai zaidi ya milioni 5 za ushuru.
Akiongea kwa niaba ya wakulima, mbali na kuipongeza serikali,Consolatha Kamenya,mkazi wa Katahoka Biharamulo,amedai huenda Kampuni ya Japan itawasaidia wakulima wengi kuendelea na kilimo cha tumbaku ambacho walianza kukata tamaa kwenye mikoa mbalimbali kutokana na kutoridhishwa na upangaji wa madaraja ya ubora pamoja na kukopwa tumbaku yao kwa zaidi ya mwaka.