Kampuni ya Simu za Mikononi ya Tigo imeingia makubaliano rasmi na kampuni ya inayojihusisha na upakuaji wa maudhui ya muziki kupitia 'APP' ya Boomplay utakaowawezesha watumiaji wa mtandao huo kufurahia burudani mbalimbali za muziki kupitia simu zao.
Akizungumza wakati wa kuutangaza ushirikiano huo jana, Meneja Chapa ya Tigo Willium Mpinga amesema kupitia huduma hiyo, watumiaji wa mtandao huo hususani wanunuzi wa vifurushi vya huduma mbalimbali watapata fursa ya kusikiliza bure nyimbo zilizopo katika APP hiyo ya Boomplay.
"Mteja atakayenunua kifurushi cha siku atapata fursa ya kufurahia nyimbo kwa siku nzima, mteja atakayejiunga na kifurushi cha wiki pia ataweza kusikiliza nyimbo bure kwa wiki nzima, vilevile kwa mteja wa mwezi naye atapata fursa hiyo kwa mwezi mzima" amesema Mpinga
Aidha amsema lengo la kufanya hivyo pamoja na mambo mengine limelenga kuwatangaza wasanii wa hapa nchini ambao baadhi yao akiwemo Hamisa Mobeto pamoja na Omary Mwanga 'Marioo' wameshiriki katika kampeni ya 'Kishua zaidi' iliyozinduliwa hivi karibuni na kampuni hiyo.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Boomplay Tanzania Natasha Stambuli Amesema idadi ya 'wapakuaji' wa 'APP' hiyo kwa hapa nchini inazidi kuongezeka siku hadi siku na kuwataka wasanii nchini kuitumia fursa hiyo kujitangaza.
Amesema kwa sasa takribani watu 20,000 wanautembelea mfumo huo kwa mwezi hapa nchini na watu 70,000 Barani Afrika ambapo na kuwasisitiza wasanii kuona kuwa hiyo ni njia sahihi ya kujiongezea kipato.
Kwa upande wao wasanii Hamisa Mobeto na Marioo walizishukuru kampuni hizo kwa kuona wanastahili kushirikiana nao kuwahamasisha wananchi kutumia huduma hizo Hulu wakiahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha malengo yanafikiwa.