KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA TMDA KATIKA KULINDA AFYA YA JAMII

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Aloyce Kamamba akizungumza katika kikao Cha kamati hiyo kujadili taarifa ya utendaji kazi ya TMDA kwa mwaka 2021/22, Jijini Dodoma mapema leo Septemba 1, 2022.


Naibu Waziri wa Afya,Mhe. Godwin Mollel akizungumza katika kikao hicho


Mkurugenzi Mtendaji wa TMDA, Bw. Adam Fimbo akizungumza katika kikao hicho


Baadhi ya Wajumbe (Wabunge) wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakiwa kwenye kikao hicho


Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeipongeza TMDA kwa kazi kubwa ya udhibiti inayofanyika katika kulinda Afya ya Jamii na kuzitaka taasisi zingine chini ya Wizara ya Afya kuiga mifumo ya utendaji iliyopo katika mamlaka hiyo.

Hayo yamebainishwa  na wajumbe wa kamati hiyo kwa nyakati tofauti wakati wakichangia na kujadili taarifa ya Utendaji Kazi ya TMDA kwa mwaka 2021/22 iliyowasilishwa bungeni Dodoma tarehe 1 Septemba, 2022.

Hata hivyo Wito umetolewa kwa TMDA kuendelea kuimarisha udhibiti katika vituo vya forodha huku mjazo ukiwa ni kusimamia na kuwezesha viwanda vya ndani vya dawa kuzalisha dawa salama, bora na fanisi.

Aidha, TMDA imetakiwa kuweka mkakati na kuimarisha utoaji elimu kwa wananchi kuanzia ngazi ya kijiji ili wananchi wapate taarifa muhimu juu ya matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Aloyce Kamamba ameishauri TMDA kuungana na taasisi nyingine za Serikali katika kufanya tafiti mbalimbali za masuala ya Afya na kuwezesha upatikanaji wa suluhisho juu ya magonjwa mbalimbali ambayo sio ya kuambukiza yanayoshamiri kwa sasa.

Nae, Naibu waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel wakati akiishukuru Kamati ya Bunge, amesema, Wizara inaendelea kutathmini huduma ya  tiba mitandaoni kabla ya kuiruhusu kuanza kufanyika nchini kutokana na mazingira ya nchi yetu. 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Bw. Adam  Mitangu Fimbo wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji Kazi mbele ya Kamati ya Kudumu  ya Bunge,  alisema,

Mamlaka pamoja na kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa mwaka 2019/20 hadi  2021/22 imeweza kutoa gawio la takriban TZS. Bilioni 14.4  katika mfuko mkuu wa Serikali, na kwamba hesabu za TMDA  zimekuwa zikikaguliwa kila mwaka na kupata hati safi kwa miaka 18 mfululizo sasa.

Mwisho.
Previous Post Next Post