Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha uwezo wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuipatia maroli 44 ambayo yatatumika kuimarisha miundombinu ya utalii ndani ya Hifadhi za Taifa.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi maroli hayo katika Hifadhi ya Taifa Mikumi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Philip Mpango ameeleza kuwa malori hayo na mitambo mingine mikubwa 18 ambayo ilishakabidhiwa itasaidia kutengeneza barabara na viwanja vya ndege kwa ajili ya matumizi ya watalii ili waweze kuona kwa urahisi vivutio mbalimbali.
Aidha, Mhe. Dkt. Philip Mpango ameongeza kuwa Serikali kupitia mradi wa Kukuza na Kuendeleza Sekta ya Utalii (REGROW) mikoa ya kusini unalenga kutoa ajira zaidi ya 40,000 kwa wakulima na wananchi wanaoishi kando kando ya hifadhi za kipaumbele, kutoa ajira nyingine ambazo sio za moja kwa moja kwa watanzania kwa ujumla pamoja na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za Taifa na vivutio vingine vya kiutamaduni na mambo kale nchini.
Awali akiuelezea mradi huo Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania yaani (REGROW) ni wa miaka sita (6) na ulianza rasmi mwaka 2017/2018 na unatekelezwa kwa gharama ya Dola za kimarekani Milioni 150.
"Mradi unatekelezwa katika maeneo ya kipaumbele ambayo ni pamoja na Hifadhi za Taifa za Ruaha, Mikumi, Udzungwa na eneo la Kaskazini la Hifadhi ya Taifa ya Nyerere (Matambwe) na Msitu wa Asili wa Kilombero (KNR).
"Maeneo yanayoguswa na mradi huo ni Wilaya ya Mbarali kwenye skimu za umwagiliaji na utunzaji wa vyanzo vya maji vya Mto Ruaha Mkuu" Aliongeza Mhe Balozi Dkt. Chana.