PROF JANABI- WANAOCHANGIA WATOTO KUPATA MATIBABU YA MOYO WANATAKIWA KUFUATA UTARATIBU.



Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Profesa Mohammed  Janabi amewataka Wananchi wanaochangia watoto kwaajili ya matibabu ya magonjwa ya Moyo kwenye mitandao ya kijamii haswa makundi ya WhatsApp  kufuata utaratibu ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza ikiwemo utapeli.

Profesa Janabi ameyasema hayo Leo Agosti 09, 2022 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya Utekelezaji wa shughuli za Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ( JKCI) na mwelekeo wa Utekelezaji kwa Mwaka wa fedha 2022-2023 .

Janabi amesema kuwa hawamkatazi mtu kuchangia ila ni vyema wakafuata utaratibu ikiwemo kupiga simu JKCI au kwenda Serikali za Mtaa ili kutambua uhalali wa mgonjwa anayeomba michango katika mitandao ya kijamii.




" kabla ya  kuanza kuchangia ni vyema mchangiaji akawasiliana na uongozi wa taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ili kupewa utaratibu mzuri wa kuchangia " amesema Prof Janabi

Kuhusu vipaumbele vya Taasisi ya Moyo na mwelekeo wa Utekelezaji kwa Mwaka wa fedha 2022-2023  Prof Janabi amesema Taasisi hiyo itaendelea kuimarisha tiba za moyo kwa kuongeza ujuzi kwa Wafanyakazi wa taasisi hiyo, kununua vifaa vya upasuaji, na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuishi maisha ya afya njema ili kuepuka kupata maradhi ya moyo.

Amesema kwa kipindi cha mwaka huu wa fedha Julai Hadi Agosti 8, 2022 wamekwisha toa huduma kwa wagonjwa 11,242 ( watu wazima 6, 242) na watoto 1600 ambapo kati ya hao 4784 ni Wanaume na 6458 ni Wanawake.

Ameongeza kuwa kwa wastani JKCI inapasua kifua kati ya wagonjwa 4-5 kwa siku na kwa kutumia tundu dogo wagonjwa kati ya 10-15 hupata huduma hiyo kwa siku.
Previous Post Next Post