MEENA: Baadhi ya vipengele vya Sheria ya Habari ya Mwaka 2016, vinailazimisha mahakama kutenda kwa matakwa ya watungaji wa sheria hiyo.



MAHAKAMA haipaswi kufungwa na sheria ya habari katika kutoa hukumu yake kulingana na uzito wa kosa alilotenda mwandishi wa habari.

Sio sawa mahakama kulazimishwa na sheria kumfunga mwandishi miaka mitatu ama zaidi hata pale kosa lake linaweza kumalizwa kwa kuonywa ama kifungo chini ya miaka hiyo.

Ni kauli ya Neville Meema, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), wakati akizungumza katika Kipindi cha Sun Down kinachorushwa na Radio Ukweli (Ukweli FM), Mjini Mrorogoro.


Amesema, baadhi ya vipengele vya Sheria ya Habari ya Mwaka 2016, vinailazimisha mahakama kutenda kwa matakwa ya watungaji wa sheria hiyo.

“Tusitunge sheria kwa ajali ya kuilazimisha mahakama kutenda kwa mujibu wa yaliyopo mioyoni mwa watunga sheria,” amesema Meena.

Akifafanua kauli yake amasema, hatua ya sheria kumuelekeza hakimu kutoa kifungo kisichopungua miaka mitatu, ni kumlazimisha asitoe hukumu chini ya kiwango hicho.


“Inawezekana hakimu akaona kosa la mwandishi linahitaji kifungo cha miaka miwili au mmoja au miezi sita na pengine miezi mitatu ama kifungo cha nje.

“Lakini kutokana na sheria hii, hakimu hawezi kutoa kifungo nje ya kile kilichoelezwa na sheria, sasa huku ni kulazimisha kila aliyetenda kosa kwenye tasnia ya habari afungwe sio chini ya miaka mitatu. Jambo hili tunaona lina ukakasi,” amesema Meena.
Previous Post Next Post