KUTUNGA SHERIA NGUMU NA KANDAMIZI HUCHANGIA KUUA USTAWI WA VYOMBO VYA HABARI



VYOMBO vya habari vinahitaji sheria rafiki zinazolenga kuimarisha mazingira ya utendaji, kutunga sheria ngumu na kandamizi, huchangia kuua ustawi wa vyombo vya habari.

Ni kauli ya Joseph Mwendapole, Mjumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), wakati akizungumza na Mhariri wa Raia Mwema, Joseph Kulangwa na Erasto Masalu, msimamizi wa kitengo cha Mwanahalisi Online.

Mjumbe huyo wa TEF alitembelea Kampuni ya Hali Halisi (MwanaHalisi, Mseto na Mawio na sasa Rais Mwema) kuzungumzia mwenendo wa machakato wa mabadiliko ya sheria za habari nchini.


Amesema, baadhi ya sheria zinazotumika kuongoza tasnia ya habari zilizotungwa mwaka 2016, zinaumiza waandishi pamoja na vyombo wanavyofanyia kazi.

“Kabla ya Nape (Waziri Nape Nnauye) kufungulia magazeti ya kampuni hii, kwa mfano gazeti la MwanHalisi lilishinda kesi mahakamani lakini pia lilimaliza muda wa kifungo chake, pamoja na yote hayo walipoomba leseni, hawakupewa.

“Hapa yametumika mamlaka ya Mkurugenzi wa Habari Maelezo aliyopewa kisheria kugoma kutoa leseni kutokana na namna anavyojisikia, haya ndio miongoni mwa mambo tunayopigania yaondolewe,” amesema Mwendapole.

Amesema, tasnia ya habari inapaswa kuwa na sheria na kanuni rafiki ili kuruhusu kukua na kwamba, kuweka sheria kali na ngumu, kunaua vyombo vya habari lakini kunaacha athari hasi kwa taifa. 

“Hatupaswi kujifungia, tunapaswa kuwa na sheria zinazokubalika ndani na nje ya nchi. Tunawezaje kutengeneza sheria za vyombo vya habari ambazo baadaye mwenyewe uliyeshiriki kutengeneza unaanza kuomba toba? ,” amesema.

Pia amesema, vyombo vya habari kwa sasa vinaweza kukosoa tofauti na miaka mitano ama sita iliyopita, lakini bado vyombo hivyo havilindwi na sheria.

“Tofauti na nyuma kidogo, kwa sasa vyombo vya habari vinaandika kwa uhuru, vinakosoa lakini kilichopo, kama mwandishi ama chombo cha habari kinawindwa, sheria hizi hizi zinatumika kuumiza chombo ama mwandishi.
“Mwandishi anaweza kufungwa kwa sheria zile zile ama chombo cha habari kinaweza kuondolewa sokoni kwa sheria hizo hizo, ndio maana tunasema uhuru wa habari lazima ulindwe kisheria,” amesema Mwendapole.

Ameeleza kuwa, mchakato wa mabadiliko ya sheria za vyombo vya habari nchini, unalenga kujenga mazingira rafiki na bora kwa wanahabari katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Pia Mwendapole ameshukuru uongozi wa Rais Samia Sukluhu Hassan, kwa kuona umuhimu na kuagiza wadau wa habari kukutana ili kupitia sheria zilizopo kwa lengo la kuimarisha tasnia ya habari nchini.
Previous Post Next Post