Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma Mhandisi Nchagwa Marwa amewakaribisha wawekezaji wa madini kuwekeza kwenye shughuli za uchimbaji wa madini kutokana na mkoa huo kuwa na madini ya aina nyingi ikiwemo ya viwanda, ujenzi, vito na metali na kusisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji.
Mhandisi Marwa ameyasema hayo leo Agosti 05, 2022 kwenye maonesho ya Nane Nane ya Kanda ya Kati yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Akizungumzia biashara ya madini katika mkoa wa Dodoma, ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imefungua masoko ya madini nchini na kusisitiza kuwa ofisi yake imejipanga kutoa leseni za biashara na vibali kwa ajili ya kusafirisha madini kwa haraka ikiwa ni mkakati wa kurahisisha shughuli za biashara ya madini.