Mchakato mabadiliko ya sheria kandamizi haulengi upendeleo kwa wanahabari



Na Humphrey Msechu

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema, mchakato wa mabadiliko ya sheria kandamizi za habari nchini, haulengi upendeleo kwa wanahabari bali haki, wajibu na mazingira mazuri ya tasia hiyo.

Amesema, malengo ya mchakato huo wa sheria za habari, ni kuwa na uhuru wa habari bila kuumiza wengine.

“Mchakato wa mabadiliko haya, unalenga kuweka mipaka lakini pia uhuru wa habari bila kuumiza mtu yeyote. Tunalenga kupata uhuru zaidi wa habari na wajibu kwa mwanahabari"

“Tunapozungumzia uhuru wa vyombo vya habari, sio kwamba tunataka upendeleo kutoka serikalini, la! Tunacholenga hapo kila mmoja apate haki na awajibike,” amesema Balile.

Kwenye kipindi hicho, Balile amesema ingawa wadau wa habari wanasimamia mabadiliko hayo, uhuru wa habari unawahusu hata wale wasio wanahabari.

Kwamba, nchi ambayo uhuru wa habari haupo, wananchi hukosa fursa ya kupata taarifa sahihi na hivyo kunyima haki yao ya msingi ya kuhabarika.

“Tufahamu kuwa uhuru wa habari ni haki ya msingi ambayo wengi wanaitaka. Vyombo vya habari visipokuwa huru, wananchi nao pia wanakosa uhuru ikiwa ni pamoja na kutoa maoni yao pia kupata taarifa zinazowahusu moja kwa moja,” amesema.

Akitoa mfano wa ajali iliyotokea Mtwara na kusababisha vifo vya wanafunzi wanane amesema, watu wamefahamu nini kimeendelea kutokana na ajali hiyo, lakini uhuru wa kutoa habari bado haujalindwa kisheria na ndio maana wadau wanataka huu ulindwe kisheria.

Amesema anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kupitia sheria za habari na kuagiza zifanyiwe maboreshio ili kuendana na mazingira yaliyopo.

“Tulikutana na rais (Rais Samia) Ikulu na kwa kuanza, tulimuomba kuhamisha tasnia ya habari na kuipeleka kwenye Wizara ya Mawasiliano, tunashukuru amefanya hivyo.

“Tukasema sasa tutengeneze muingiliano mzuri wa sheria, na jambo zuri ni mchakato umeanza lakini siku za karinbuni hapa, umepoa, ” amesema.

Ametumia nafasi hiyo kumkumbusha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kuongeza kasi ili kufikia matamanio ya wadau wa tasnia ya Habari
Previous Post Next Post